Wakulima wametakiwa kuzingatia upimaji wa afya ya udongo kabla ya kutumia mbolea ili kubaini virutubisho vinavyohitajika na kuchagua aina inayofaa kwa mazao yao, hatua inayolenga kuongeza tija ya kilimo na uzalishaji wa chakula.
Yohana Masalapilu, Mtaalamu wa Maabara kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Kanda ya Kaskazini, amesema mkulima anapaswa kuanza kwa kufahamu hali ya udongo wake badala ya kuamua aina ya mbolea kwa mazoea bila kujua mahitaji halisi ya shamba lake.
Akizungumza katika Maonesho ya Siku ya Chakula Duniani Kitaifa yanayofanyika jijini Tanga kuanzia Oktoba 10 hadi 16, 2026, sambamba na maadhimisho ya siku ya Mbolea Duniani Oktoba 13, amesema upimaji wa udongo humwezesha mkulima kutambua kiwango cha asidi na virutubisho vilivyopo, hivyo kusaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu aina na kiasi cha mbolea ya kutumia.
Ameongeza kuwa matumizi ya muda mrefu ya ardhi yanaweza kupunguza virutubisho muhimu kwa ukuaji wa mimea, hivyo ni muhimu kupima udongo ili kubaini upungufu na kuchagua mbolea inayokidhi mahitaji ya zao husika. Kwa kufanya hivyo, mkulima anaweza kuepuka matumizi yasiyo sahihi ya mbolea na kuboresha tija ya uzalishaji.
Amewahimiza wakulima kutumia fursa ya maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani, ili kupata elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea kwa kutembelea banda la TFRA katika maonesho hayo, yanayoendelea sambamba na maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kwenye viwanja vya shule ya Sekondari Usagara Jijini Tanga, yenye lengo la kuhamasisha juhudi za kuboresha uzalishaji na upatikanaji wa chakula.


No comments:
Post a Comment