
Na Mwandishi Wetu - Dar es salaam
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga (Mb), amezindua huduma ya Bongo kama China itakayowawezesha wafanyabiashara kuagiza na kufanya malipo hapa mchini bila kubadilisha fedha za kigeni kwa ajili ya bidhaa kutoka nchini China.
Waziri Kapinga amesema mfumo huo wa kidijitali una lengo la kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kidijitali katika malipo na miamala ya kibiashara kwa wafanyabiashara na sekta binafsi kwa lengo la kuongeza ufanisi na usalama kwa wafanyabiashara.
Aliongeza kuwa mfumo huu uliobuniwa na benki ya Stanbic kwa wanyabiashara wa kariakoo, ni chachu ya kuleta mabadiliko na utanusuru fedha za kigeni ambazo zitatumika kwa ajili ya shughuli nyingine za mauzo na manunuzi ya nje.
Awali akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika kwenye soko la Kariakoo,mwakilishi wa Mkurugenzi wa Benki ya Stanbic Bwana Jonath Ngoma amesema, waliamua kuja na huduma hii kwa lengo la kuwapunguzia adha wafanyabiashara kubeba fedha nyingi kwa wakati mmoja sambamba na kuepuka vikwazo, muda na kudhulumiwa.
Amesema huduma hii itamsaidia mfanyabiashara kupata risiti kwa wakati na kuwa na kumbukunbu sahihi za biashara na kupunguza mlolongo wa ucheleweshaji.
Hafla hiyo iliandaliwa na benki ya Stanbic kwa kushirikiana na Wasafi Media na jumuiya ya wafanyabiashara wa soko la kariakoo, Mkuu wa wilaya ya Ilala Edward Mpogole na Diwani wa kariakoo Hajji Manara na umoja wa wafanyabiashara maarufu kama Wamachinga.




No comments:
Post a Comment