Na. Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Wadau wa sekta ya afya wapewa mafunzo ya siku nne jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 26 hadi 29 Oktoba, 2026, yaliyolenga kuwajengea uelewa kuhusu Kinga Dhidi ya Unyonyaji, Ukatili wa Kingono na Unyanyasaji (Protection from Sexual Exploitation, Abuse and Harassment – PSEAH) ili kuendelea kulinda haki, utu na usalama wa wananchi wanaonufaika na huduma za afya.
Warsha hiyo inalenga kuimarisha mifumo ya ulinzi, uwajibikaji na maadili katika utekelezaji wa programu zinazofadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund) na ni sehemu ya juhudi za kujenga uwezo wa taasisi kuzuia vitendo vya unyonyaji, ukatili na unyanyasaji wa kingono, kuweka mifumo madhubuti ya kuripoti matukio, na kuhakikisha manusura wanapata msaada unaozingatia mahitaji yao.
Serikali, kwa kushirikiana na Mfuko wa Dunia, inaendelea kuimarisha usimamizi, uratibu na uwajibikaji katika utekelezaji wa programu hizo, huku ikihakikisha zinazingatia viwango vya juu vya uadilifu na maadili.
Maeneo makuu yaliyotiliwa mkazo wakati wa warsha hiyo ni pamoja na kuimarisha uwezo wa viongozi na wajumbe wa Kamati ya Taifa ya Uratibu wa Mfuko wa Dunia (TNCM) katika usimamizi, utawala unaozingatia maadili, na uwajibikaji katika utekelezaji wa PSEAH na sehemu ya pili inahusisha Wizara ya Fedha kama Mpokeaji Mkuu wa Ruzuku (Principal Recipient – PR), Wizara ya Afya kama Mpokeaji Kiongozi wa Ruzuku Ndogo (Lead Sub-Recipient - LSR), pamoja na wapokeaji wengine wa ruzuku ndogo, kwa lengo la kuimarisha mifumo ya ulinzi ndani ya taasisi zao.
Vilele, inajikita katika utekelezaji salama wa programu, hususan kutathmini na kupunguza hatari za unyonyaji, ukatili na unyanyasaji wa kingono katika ngazi ya utoaji huduma.
Miongoni mwa viongozi walioshiriki warsha hiyo ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) na Mwenyekiti wa TNCM, Dkt. Jim Yonazi, Makamu Mwenyekiti wa TNCM, Godlisten Moshi, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Prof. Tumaini Nagu, Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI, Dkt. Adam Mrisho na Katibu Mtendaji wa TNCM, Kent Pius.








No comments:
Post a Comment