
Wahitimu wa Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT Academy) wameaswa kutumia maarifa waliyoyapata chuoni hapo kutafuta masuluhisho ya changamoto zinazowakabili wananchi na taasisi za fedha.
Hayo yamesemwa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, wakati wa Mahafali ya Tano ya BoT Academy ya wahitimu wa Stashahada ya Uendeshaji na Usimamizi wa Benki na Stashahada ya Uzamili katika Uongozi wa Benki yaliyofanyika tarehe Oktoba 30, 2026 jijini Mwanza.
“Nawahimiza kutumia maarifa yenu kutafuta suluhisho za changamoto zinazowakabili wananchi na taasisi za fedha”. Alisema
Aidha, aliwataka wahitimu hao kutumia teknolojia mpya ikiwemo ile ya Akili Unde, kufanya kazi kwa ushirikiano na kushiriki katika kujenga mazingira ya kifedha yaliyo salama, jumuishi na yenye ufanisi.
Kwa upande wake, Naibu Gavana wa BoT ambaye pia ni Mweneyekiti wa Bodi ya Chuo cha Benki Kuu, Dkt. Rahma Mahfoudh, alisema Chuo hicho kimepiga hatua kubwa hususan kupitia mageuzi yaliyofanyika katika muundo, majukumu na mwelekeo wa kimkakati wa Chuo.
Aliongeza kuwa mabadiliko hayo yameimarisha uwezo wa Chuo katika kutoa mafunzo yenye ubora, kukuza weledi na maadili ya kitaaluma, pamoja na kupanua wigo wa huduma za mafunzo kwa sekta ya fedha na benki nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Mahafali hayo yalitanguliwa na Kongamano la Kitaaluma la siku mbili lililojadili Namna Akili Unde inavyobadili utendaji wa Benki Kuu na benki za biashara (“Beyond Digital Transformation: How Artificial Intelligence is Reinventing Banks and Central Banks”)













No comments:
Post a Comment