WATOTO 751 WAFIKIWA NA PROGRAMU ZA ELIMU NYUMBANI NA HOSPITALINI - PROF. MKENDA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, October 16, 2026

WATOTO 751 WAFIKIWA NA PROGRAMU ZA ELIMU NYUMBANI NA HOSPITALINI - PROF. MKENDA



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA




Serikali imeanzisha programu za shule za nyumbani zinazohudumia wanafunzi 691 na shule za hospitalini zinazowafikia wanafunzi 60, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha watoto wenye changamoto za kiafya na ulemavu wanaendelea kupata elimu hata wanaposhindwa kuhudhuria masomo shuleni.


Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Nne wa Kitaifa wa Elimu Jumuishi wa mwaka 2026/27 hadi 2030/31 uliozinduliwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, sambamba na miongozo tisa ya kitaifa na ugawaji wa vifaa saidizi vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 730.




Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo leo Oktoba 16,2026 jijini Dodoma, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia jijini Dodoma, Waziri wa wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda, amesema Serikali inalenga kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya elimu bila kujali ulemavu au changamoto nyingine zinazoweza kuathiri ushiriki wake katika masomo.

Amesema kupitia programu hizo, watoto ambao hali zao za kiafya zinawazuia kufika shuleni wanapata nafasi ya kuendelea na masomo, hatua inayolenga kupunguza pengo la upatikanaji wa elimu na kuwapa fursa ya kutimiza ndoto zao.

Katika kuimarisha juhudi hizo, Serikali imetoa vifaa saidizi vya kidijitali na kimwili, vikiwemo kompyuta mpakato 200, tableti 240 na vifaa vyenye thamani ya Shilingi milioni 200 kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika vyuo vikuu.

Vifaa hivyo vinatarajiwa kuwasaidia wanafunzi kutumia teknolojia katika kujifunza, kupata taarifa na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kielimu kulingana na mahitaji yao.

Profesa Mkenda amesema Serikali pia imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 12 katika kuboresha miundombinu ya shule jumuishi za mfano, majengo na shule kongwe za elimu maalumu, pamoja na kuwezesha mafunzo kwa watumishi 2,058, wakiwemo walimu wa elimu maalumu 1,276, walimu wenye ulemavu 242, walezi na Mawadeni 316.

Aidha, zaidi ya vitabu 522,000 vya Breli na maandishi yaliyokuzwa vimechapishwa ili kuwawezesha wanafunzi wenye ulemavu wa kuona kupata nyenzo zinazokidhi mahitaji yao ya kujifunzia.

Katika hatua nyingine, Serikali imefanya mafunzo ya Lugha ya Alama ya Tanzania kuwa ya lazima kwa walimu wote tarajali nchini ili kuongeza uwezo wao wa kuwasiliana na kuwafundisha wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia.

Pia, vyuo vinavyotoa mafunzo ya elimu maalumu vimeongezeka kutoka kimoja hadi vitatu, huku walimu tarajali 2,000 wakipatiwa ufadhili wa kusoma shahada ya elimu maalumu. Taasisi za elimu ya juu zinazotoa huduma kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu nazo zimeongezeka kutoka moja hadi 19.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Sekiboko, amewataka wanafunzi wenye ulemavu kujiamini na kutumia vifaa saidizi walivyopatiwa katika kuboresha masomo yao, akisisitiza kuwa ulemavu si kikwazo cha kufikia mafanikio.

Sekiboko ametoa mfano wa Mbunge Yumna, ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo, akisema amekuwa akitumia nafasi yake kuwasemea watu wenye ulemavu katika vikao vya Bunge na kamati.

Amesema wanafunzi wakitumia vifaa hivyo kwa usahihi, wakajituma katika masomo na kujiwekea malengo, wanaweza kufikia nafasi mbalimbali za uongozi na kutoa mchango mkubwa kwa taifa.

Ameitaka Wizara ya Elimu kuhakikisha mpango wa ugawaji wa vifaa saidizi unakuwa endelevu na kuwafikia wanafunzi wengi zaidi katika mikoa yote nchini, huku akieleza kuwa Bunge litaendelea kusimamia na kuunga mkono juhudi za kuboresha elimu jumuishi.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyuma katika kupata haki ya elimu.

Amebainisha kuwa ugawaji wa vifaa saidizi uliofanyika ni mara ya tatu katika mwaka huu wa kalenda, akiwashukuru viongozi wa Serikali na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kwa ushirikiano wao katika kuendeleza elimu nchini.

Kwa upande wa Mwakilishi wa Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) Ayubu Kafikilo amesema kwa kushirikiana na Serikali ya Canada, wametoa kompyuta mpakato 200 na tableti 240 kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi wenye ulemavu kunufaika na teknolojia ya kidijitali.

Amesema UNICEF pia inaendelea na maandalizi ya upatikanaji wa vifaa vingine saidizi, vikiwemo vifaa vya Breli, vifaa vya kusaidia kusikia, magongo na viti vya magurudumu.

Vilevile, shirika hilo linashirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kubadilisha vitabu vya kawaida vya mtaala kuwa vitabu vya kidijitali vinavyoweza kutumiwa na wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwa kutumia teknolojia za kisasa, ikiwemo akili bandia.

Mkakati huo unaambatana na miongozo tisa ya kitaifa inayohusu mafunzo kwa walimu, matumizi ya TEHAMA na teknolojia saidizi, Lugha ya Alama ya Tanzania, elimu ya amali, huduma kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu na matumizi ya Breli ya Kiswahili.

Profesa Mkenda ametoa wito kwa wazazi na jamii kuacha kuwaficha watoto wenye ulemavu majumbani na badala yake kuwawezesha kupata elimu na kushiriki katika shughuli za kijamii.







No comments:

Post a Comment