WAZIRI HOMERA AIPONGEZA REA KWA VITENDO KATIKA MAPINDUZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, October 24, 2026

WAZIRI HOMERA AIPONGEZA REA KWA VITENDO KATIKA MAPINDUZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA


Na Mwandishi Wetu - Namtumbo


Waziri wa Nishati na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Mhe. Juma Homera, ameipongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuendelea kutekeleza kwa vitendo juhudi za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwemo kutoa majiko banifu 400 na mitungi ya gesi 600 katika mashindano ya Site Trust Nishati Safi Marathon 2026 yaliyofanyika wilayani Namtumbo, mkoani Ruvuma.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa mashindano hayo katika viwanja vya Shule ya Msingi Namtumbo, leo Oktoba 24, 2026, Mhe. Homera amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mha. Hassan Saidy, kwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Amesema ushiriki wa REA katika mashindano hayo unaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata elimu na fursa za kutumia nishati safi ya kupikia, hatua inayolenga kulinda afya zao, kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa pamoja na kuhifadhi mazingira.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Bw. Rajabu Mbega, ameipongeza REA kwa kuendelea kuhamasisha wananchi kutumia nishati safi ya kupikia, huku akisisitiza umuhimu wa jamii kubadili mifumo ya upishi na kuanza kutumia nishati safi, salama na rafiki kwa mazingira.

Naye, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa REA, Bi. Martha Chassama, amesema Wakala utaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na kuhamia kwenye nishati safi ya kupikia.

Amesema utoaji wa majiko banifu na mitungi ya gesi katika mashindano hayo ni sehemu ya juhudi za REA za kuongeza matumizi ya teknolojia za nishati safi ya kupikia, sambamba na kuunga mkono utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kuongeza matumizi ya nishati hiyo nchini.

Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Site Trust chini ya kaulimbiu “Nishati Safi ya Kupikia, Okoa Afya na Mazingira” yamelenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia katika kulinda afya, kuhifadhi mazingira na kuboresha maisha ya jamii.

No comments:

Post a Comment