Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, amezitaka nchi za Afrika kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika uwekezaji wa viwanda vya kuongeza thamani madini ili kutumia utajiri wa rasilimali zilizopo barani humo kujenga uchumi wa viwanda, kuongeza ajira na kukuza ustawi wa wananchi.
Akizungumza wakati wa kufunga Mkutano wa Kimataifa wa Madini na Uwekezaji Tanzania (TMIC 2026), uliofanyika kwa siku tatu kuanzia Novemba 19 hadi 21, 2026, jijini Dar es Salaam, Mhe. Othman amesema Afrika inapaswa kuelekeza nguvu katika kujenga viwanda vya ndani vya kuchakata madini na kuzalisha bidhaa kamili badala ya kuendelea kutegemea usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi.
Amesema uwekezaji katika viwanda vya kuzalisha betri, vifaa vya umeme na bidhaa nyingine zinazotumia madini ni fursa muhimu kwa mataifa ya Afrika, hususan katika kipindi hiki ambacho dunia inaelekea katika matumizi ya nishati safi na teknolojia za kisasa.
Ameeleza kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za madini ya kimkakati, yakiwemo Graphite, Nickel, Shaba, Rare Earth Elements, Niobium, Dhahabu, Tanzanite, Almasi na Rubi, ambazo zina umuhimu mkubwa katika teknolojia za kisasa, utengenezaji wa vifaa vya kielektroniki na nishati safi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwapatia mitaji, teknolojia sahihi na huduma za kitaalamu ili kuongeza uzalishaji, kuboresha shughuli za uchimbaji na kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira.
Amesema mijadala ya TMIC 2026 imekuwa na manufaa makubwa kwa kuwakutanisha wadau wa sekta ya madini kutoka ndani na nje ya nchi, kujadili changamoto za uongezaji thamani madini, upatikanaji wa mitaji, ushiriki wa jamii na matumizi ya teknolojia za kisasa.
Katika hatua nyingine, Mhe. Othman ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imefanikiwa kutekeleza utafiti wa jiolojia katika visiwa vya Unguja na Pemba na kukamilisha ramani ya jiolojia inayoonesha aina mbalimbali za miamba na madini yanayopatikana katika maeneo hayo.
Amesema hatua hiyo inafungua fursa mpya za uwekezaji katika shughuli za utafiti na uchimbaji wa madini Zanzibar, huku akiwakaribisha wawekezaji kutembelea visiwa hivyo na kuchunguza fursa zilizopo.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kutekeleza mikakati madhubuti ya kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha Watanzania kupitia uongezaji thamani ndani ya nchi.
Amesema Serikali imeimarisha mfumo wa kisheria kwa kuweka masharti yanayozuia usafirishaji wa madini nje ya nchi bila kuongezwa thamani, akieleza kuwa Kifungu cha 133(1) hadi (5) cha Sheria ya Madini, Sura ya 123, kinaweka msingi wa kuhakikisha madini yanaongezwa thamani nchini kabla ya kusafirishwa.
Ameongeza kuwa Serikali imeweka pia kanuni zinazobainisha viwango vya uongezaji thamani kwa kila aina ya madini kabla hayajasafirishwa nje ya nchi, hatua inayolenga kuhakikisha nchi inapata manufaa makubwa zaidi kutokana na rasilimali zake.
Mhe. Mavunde amesema pamoja na kuweka mfumo huo wa kisheria, Serikali inatekeleza mikakati ya kuhakikisha wawekezaji wana uhakika wa upatikanaji wa malighafi zitakazotumika katika viwanda vya kuongeza thamani madini.
Ameeleza kuwa Serikali imejipanga kuongeza maeneo ya utafiti wa kina wa madini ili kutambua maeneo mapya yenye rasilimali na kuongeza upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda vinavyoanzishwa nchini. Aidha, amesema asilimia 10 ya mapato yatokanayo na sekta ya madini inaelekezwa katika shughuli za utafiti wa madini.
Akizungumzia mazingira ya uwekezaji, Mhe. Mavunde amesema upatikanaji wa nishati ya uhakika ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali katika kuvutia na kuwezesha uanzishwaji wa viwanda vya kuongeza thamani madini.
Amesema Tanzania imejipanga kufikia uwezo wa kuzalisha megawati 8,000 za umeme ifikapo mwaka 2030, huku Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere ukiwa na uwezo wa kuzalisha megawati 2,115. Ameeleza kuwa Serikali inaendelea na mikakati ya kuongeza uzalishaji wa umeme ili kukidhi mahitaji ya viwanda na shughuli nyingine za kiuchumi.
Vilevile, amesema Serikali imeandaa eneo maalumu la uwekezaji katika eneo la mgodi wa zamani wa Buzwagi, Kahama mkoani Shinyanga, lenye ukubwa wa ekari 1,331, ambalo sasa limegeuzwa kuwa Eneo Maalumu la Kiuchumi la Buzwagi (Buzwagi Special Economic Zone).
Amesema eneo hilo limeandaliwa kwa ajili ya kuvutia wawekezaji kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani madini, huku lengo likiwa ni kuongeza ajira na shughuli za kiuchumi katika eneo hilo na nchini kwa ujumla.
Katika kuboresha usafirishaji wa madini na malighafi kwa ajili ya viwanda, Mhe. Mavunde amesema Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, ikiwemo bandari, reli na barabara, ili kuwezesha madini kutoka maeneo ya uzalishaji kufikishwa kwa urahisi katika viwanda na masoko.











No comments:
Post a Comment