Imekuwa saa, siku, mwezi hadi kufikia miaka 40 ya kuwepo kwa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ambapo inaadhimisha miaka ya uimarishaji mifumo ya kutambua na kusukuma mbele bunifu na Teknolojia zinazoanzishwa nchini pamoja na kuimarisha utafiti kwa maendeleo ya taifa.
Maadhimisho hayo yanafikia kilele Novemba 17 na 18, 2026 ambapo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba atakuwa mgeni Rasmi katika hitimisho hilo katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam,
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Novemba 11, 2026, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema maadhimisho hayo yaliyozinduliwa Julai 2 mwaka huu yamehusisha shughuli mbalimbali, ikiwemo kliniki za ubunifu, maonesho mbalimbali ya ubunifu ikiwemo katika viunga vya Bunge na pia kufanyika kwa tathmini ya mchango wa COSTECH na mwelekeo wa kiutekelezaji kuwezesha kufikia DIRA 2050 kutumia sayansi, teknolojia na ubunifu.
Amesema miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na bunifu mbalimbali zilizoibuliwa na Watanzania kuendelezwa na kuwezeshwa kuingia sokoni akitolea mifano ya bunifu hizo kuwa ni Mkanda Salama unaosaidia kudhibiti kutokwa damu nyingi kwa mama baada ya kujifungua, chanjo ya samaki inayolenga kupunguza vifo vinavyotokana na magonjwa na teknolojia ya kutengeneza saruji kwa gharama nafuu kwa kutumia pozolana na chokaa.
Prof. Mkenda amesema baadhi ya bunifu hizo zimeanza kufikia hatua za uzalishaji na kufanya mazungumzo na wawekezaji, huku nyingine zikiendelea kufanyiwa tathmini ya usalama, ubora na gharama za uzalishaji kabla ya kuingia sokoni.
Aidha, amesema maadhimisho hayo yamekuwa jukwaa la kuimarisha matumizi ya sayansi katika sekta mbalimbali, ikiwemo afya, kilimo uvuvi ufugaji na nyingine.
"Tumeanza kwa mijadala na wadau wa sekta mfano kongamano la kuendeleza sayansi katika tiba asili lililowakutanisha watafiti na wadau wa tiba kujadili namna ya kutumia tafiti za kisayansi kuthibitisha ufanisi na usalama wa dawa zinazotokana na mimea" amesema Mkenda.




No comments:
Post a Comment