KADOGOSA AITAKA TBA KUSHIRIKISHA SEKTA BINAFSI KUONGEZA THAMANI YA RASILIMALI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, November 11, 2026

KADOGOSA AITAKA TBA KUSHIRIKISHA SEKTA BINAFSI KUONGEZA THAMANI YA RASILIMALI


Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, ameitaka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kuongeza kasi ya uendelezaji na matumizi ya rasilimali zake kwa kushirikisha sekta binafsi, wawekezaji na taasisi za kifedha ili kuongeza ufanisi wa utendaji na kuiwezesha taasisi hiyo kujitegemea kifedha ndani ya muda mfupi.

Waziri Kadogosa ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara yake katika Wakala huo jijini Dar es Salaam, ambapo alipokea taarifa kuhusu hali ya rasilimali zinazomilikiwa na TBA, mikakati ya utekelezaji wa majukumu yake pamoja na changamoto zinazoikabili taasisi hiyo.

Waziri Kadogosa amesisitiza umuhimu wa kufanya tathmini ya kina ya mali zote zinazomilikiwa na TBA ili kubaini thamani yake halisi na kuweka mikakati madhubuti ya kuziendeleza na kuzitumia katika kuongeza mapato ya taasisi hiyo.

Amesema kuwa, licha ya awali thamani ya rasilimali za TBA kukadiriwa kuwa kati ya shilingi bilioni 400 na 600, tathmini iliyofanyika katika mikoa takribani 10 imebaini kuwa thamani ya mali hizo inafikia shilingi trilioni 1.4. Hali hiyo inaonesha uwepo wa fursa kubwa za kiuchumi ambazo zinapaswa kutumiwa ipasavyo.

Ameelekeza tathmini hiyo kuendelea katika maeneo yote yanayomilikiwa na wakala huo ili kubaini thamani halisi ya rasilimali zake, ambayo inatarajiwa kuwa zaidi ya shilingi trilioni mbili hadi tatu.

Aidha, Waziri Kadogosa amesema Serikali inalenga kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ambapo takribani asilimia 70 ya utekelezaji wa mipango hiyo unatarajiwa kutegemea ushiriki wa sekta binafsi kupitia mifumo mbalimbali ya ushirikiano.

Ameeleza kuwa TBA inapaswa kujifunza kutokana na mageuzi yaliyofanyika katika sekta ya bandari kupitia ushirikishwaji wa sekta binafsi, ambayo yamechangia kuongeza ufanisi wa shughuli za bandari na kuchochea mahitaji ya miundombinu mingine ya usafirishaji, ikiwemo barabara.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), FRV. Said Mndeme, amesema wakala huo umejipanga kutekeleza maelekezo ya Waziri kwa kufanya mageuzi katika mifumo ya uendeshaji wa taasisi hiyo, ikiwemo kuandaa mifumo ya ushirikiano na wawekezaji, wakandarasi pamoja na taasisi za kifedha.

Mndeme amesema ushirikiano huo utasaidia kuharakisha uendelezaji wa maeneo yanayomilikiwa na TBA, kuongeza thamani ya rasilimali zake, kupanua wigo wa mapato na kuiwezesha taasisi hiyo kufikia lengo la kujitegemea kifedha ndani ya muda uliopangwa.

No comments:

Post a Comment