Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi, ametaka kuharakishwa kwa usanifu wa upanuzi wa mradi wa maji wa Kilwa ili wananchi wa Mandawa, Hoteli Tatu na maeneo jirani nao wanufaike na huduma ya maji safi na salama.
Akizungumza wakati wa kukagua mradi huo katika eneo la Mavuji, Wilaya ya Kilwa akiwa ziarani mkoani Lindi, Makamu wa Rais amesisitiza kuwa uwekezaji wa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan unapaswa uwafikie pia wananchi ambao bado wanakabiliwa na changamoto ya maji.
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amesema mamlaka ya maji imeelekezwa kuanza usanifu ili kubaini gharama za upanuzi, huku wizara ikiahidi kutoa fedha za kufanikisha hatua hiyo.
Mradi huo, ambao ni sehemu ya Mradi wa Maji wa Miji 28, una thamani ya takribani shilingi bilioni 44.25 na umefikia asilimia 97.4 ya utekelezaji. Tayari umeanza kutoa huduma na unatarajiwa kunufaisha wananchi takribani 59,983 wa Kilwa Masoko, Kilwa Kivinje, Mavuji na Mchakama.
Ukitumia chanzo cha Mto Mavuji, mradi huo una uwezo wa kuzalisha lita milioni tano kwa siku. Pia unahudumia Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko, inayohitaji lita milioni moja kwa siku wakati wa uendeshaji wake.







No comments:
Post a Comment