Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Rhimo Nyansaho (Mb), amesisitiza umuhimu wa elimu katika kuwawezesha wanawake na wasichana kutambua uwezo wao, kukuza vipaji na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
Akizungumza akiwa Mgeni Rasmi katika mahafali ya Kidato cha Sita ya Shule ya Wasichana Canossa, iliyopo Tegeta Kibaoni, jijini Dar es Salaam, tarehe 14 Novemba 2026, Dkt. Nyansaho ameipongeza shule hiyo kwa kutimiza miaka 20 ya kutoa elimu bora na kuwalea mabinti katika misingi ya imani, maadili, nidhamu na uwajibikaji.
Amesema falsafa ya shule hiyo ya kumjenga mtoto wa kike kiroho, kitaaluma na kimaadili ni mchango muhimu katika kuandaa kizazi cha wanawake wenye uwezo wa kuwa viongozi na washiriki madhubuti wa maendeleo ya jamii na Taifa.
Aidha, Dkt. Nyansaho amebainisha kuwa mafanikio ya wahitimu hao yanaakisi hatua zilizopigwa na Tanzania katika kupanua fursa za elimu na uwezeshaji wa wanawake, akitolea mfano wa kihistoria wa kuapishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 19 Machi 2021, kuwa Rais wa kwanza mwanamke nchini.
Amesema uongozi wa Rais Dkt. Samia unaendelea kuthibitisha uwezo mkubwa wa wanawake katika kushika nafasi za juu za uongozi na kufanya maamuzi yanayochochea maendeleo ya Taifa.
Amewahimiza wahitimu kujenga uwezo wao kupitia elimu, bidii, nidhamu, uadilifu na uthubutu, akisisitiza kuwa maendeleo ya Tanzania yanahitaji ushiriki na mchango wa kila Mtanzania, bila kujali jinsia.
Katika kuzungumzia masuala ya ulinzi na usalama wa Taifa, Waziri Nyansaho amesisitiza kuwa jukumu la kulinda amani, umoja na mshikamano wa nchi si la vyombo vya ulinzi na usalama pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi.
Ameeleza kuwa uzalendo wa kweli hujidhihirisha kupitia kuheshimu sheria, kupinga rushwa, kulinda mali za umma na mazingira, kujiepusha na vitendo vya uhalifu na kushiriki katika kudumisha umoja wa kitaifa.
Aidha, amewataka vijana kuwa kizazi chenye maarifa ya kisasa, ubunifu na uwezo wa kutumia teknolojia katika kutatua changamoto za maendeleo, akisisitiza kuwa amani ni msingi wa maendeleo endelevu na ni wajibu wa kila mmoja kuitunza.
Ameongeza kuwa wahitimu wanapaswa kuwa tayari kushiriki katika mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa na Serikali, akieleza kuwa mafunzo hayo huwajengea vijana uzalendo, nidhamu, uongozi, stadi za kazi, uwezo wa kushirikiana na kujitegemea.
Vilevile, Dkt. Nyansaho amewahimiza wahitimu kutazama mafunzo ya JKT kama fursa ya kujijenga kimwili, kiakili na kimaadili, pamoja na kuimarisha misingi ya umoja na mshikamano wa kitaifa kwa kuishi na kushirikiana na vijana kutoka maeneo na mazingira mbalimbali ya nchi.
Amewataka pia kutokutegemea ajira pekee baada ya kuhitimu elimu ya juu, bali kujifunza kutambua na kutumia fursa zilizopo, kuanzisha shughuli za uzalishaji mali, kutumia teknolojia kukuza biashara na kutengeneza ajira kwa wengine.
Amesema Tanzania inahitaji vijana wenye maarifa, ubunifu, maadili mema na uwezo wa kujitegemea kiuchumi ili kuimarisha ustawi wa jamii na usalama wa Taifa kwa muda mrefu.










No comments:
Post a Comment