Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema Serikali imetenga shilingi milioni 760 kwa ajili ya kulipa fidia wananchi wa Mkoa wa Lindi ambao maeneo yao yamepitiwa na mradi wa bomba la gesi asilia, ambapo malipo hayo yanatarajiwa kufanyika ifikapo Januari 2027.
Mhe. Salome ameeleza kuwa tathmini ya maeneo husika tayari imekamilika, akibainisha kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha wananchi hao wanapata stahiki zao kwa wakati.
Amesema hayo akiwa katika Kata ya Madangwa, ambako Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisimama kuwasalimia wananchi wakati akiendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Lindi.
Aidha, Mhe. Salome amesema Wizara ya Nishati imeandaa shilingi bilioni 5.7 kwa ajili ya kulipa fidia wananchi ambao maeneo yao yamepitiwa na mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Masasi hadi Mahumbika.
Ameeleza kuwa fedha hizo zipo katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu za kutolewa ili wananchi ambao bado hawajalipwa waweze kupata fidia zao.
Katika hatua nyingine, Mhe. Salome ameelekeza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kufanya uchunguzi wa mashamba ya wananchi yaliyoharibiwa na magari yanayohusika na utekelezaji wa mradi wa bomba la gesi, ili kubaini kiwango cha uharibifu na kuweka utaratibu wa kuwalipa fidia stahiki.




No comments:
Post a Comment