MRADI WA LNG LINDI NI WA KIELELEZO AFRIKA – NDEJEMBI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, November 15, 2026

MRADI WA LNG LINDI NI WA KIELELEZO AFRIKA – NDEJEMBI


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema kuwa Mradi wa Kuchakata na Kusafirisha Gesi Asilia Kimiminika (LNG) unaotarajiwa kutekelezwa mkoani Lindi ni mradi wa kimkakati na wa kielelezo katika ukanda wa Afrika Mashariki na bara la Afrika kwa ujumla.

Mhe. Ndejembi ameyasema hayo wakati wa ziara yake mkoani Lindi, alipokuwa akizungumza na wananchi wa mkoa huo, ambapo ameeleza kuwa mradi huo umefikia hatua za mwisho kuelekea kuanza kutekelezwa na unatarajiwa kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa Lindi na kuleta manufaa mbalimbali kwa wananchi.

Ametoa mfano wa wananchi wa Likong'o ambao tayari wamenufaika na shughuli za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), lililojenga shule ya msingi kwa ajili ya jamii hiyo.

Aidha, Makamu wa Rais ameeleza kuwa Serikali imetekeleza na kukamilisha masharti na mahitaji yaliyokuwa yamewekwa na mwekezaji ili kuwezesha mradi huo kuanza, huku akieleza kuwa hatua inayofuata ni kwa kampuni zinazohusika kuhakikisha utekelezaji wa mradi unaanza.

Amewatoa hofu wananchi wa Lindi na Watanzania kwa ujumla kuhusu mustakabali wa mradi huo, akibainisha kuwa Serikali imekamilisha sehemu yake ya maandalizi.

Kuhusu mikataba ya uwekezaji, Mhe. Ndejembi amesema kuwa Serikali imekamilisha majadiliano na kuwasilisha mikataba hiyo kwa kampuni zinazotarajiwa kuwekeza ili ziipitie na kujiridhisha kabla ya hatua zinazofuata.

Amesisitiza kuwa mradi wa LNG unatarajiwa kuwa lango muhimu la ukuaji wa uchumi kusini mwa Tanzania, kuongeza fursa za uwekezaji na kuchochea maendeleo ya wananchi hao.

No comments:

Post a Comment