Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi, ametua jijini London, Uingereza, kwa ajili ya kushiriki Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya WTM London 2026 yanayotarajiwa kufanyika Novemba 3–5, 2026.
Katika siku ya kwanza ya ziara yake, akiwa katika Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza, Dkt. Kijaji leo Novemba 2, 2026 amekutana na kufanya mazungumzo na wadau mbalimbali wa utalii kwa lengo la kujadili fursa na mikakati ya kukuza na kuitangaza Tanzania kama kituo cha utalii katika soko la kimataifa.
Katika mazungumzo hayo, Dkt. Kijaji amepokea wasilisho kuhusu utalii kutoka kwa Bw. Tim Henshall, Afisa anayeshughulikia masuala ya Utalii katika Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza (Tanzania High Commission UK).
Aidha, amekutana na kufanya mazungumzo na Bw. Craig Rix, Mtendaji Mkuu wa Gecko Publishing, ambapo wamejadili fursa za kuitangaza Tanzania kupitia machapisho ya Gecko Publishing, ikiwemo jarida la Travel Africa Magazine, ili kuongeza mwonekano wa vivutio vya utalii vya Tanzania katika masoko ya kimataifa.
Katika kikao kingine, Dkt. Kijaji amekutana na Bw. George Bartlam, Meneja wa Mauzo ya Ubia wa Klabu ya Soka ya Brentford (Brentford Football Club) ambayo kwa sasa inashika nafasi ya 6 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ambapo wamejadili uwezekano wa kutumia klabu hiyo kuitangaza Tanzania.
Vikao hivyo vimehudhuriwa pia na Mwakilishi wa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Bw. Patrick Mwakalobo na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Dkt. Thereza Mugobi.












No comments:
Post a Comment