Na Mwandishi Wetu, TANGAMwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, Rajabu Abdurahmani, amesema kuwa ujenzi wa chama imara unahitaji uwepo wa watendaji wenye mazingira mazuri ya kufanyia kazi, ikiwemo kuwa na makazi ya kudumu katika ofisi za chama wilayani.
Abdurahmani amesema kuwa ili CCM iendelee kuwa na uwezo wa kusimamia majukumu yake, watendaji wa chama katika ngazi za wilaya wanapaswa kuishi katika nyumba za CCM ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao bila changamoto zinazotokana na gharama za kupanga makazi.

Amesema kuwa katika kutekeleza azma hiyo, walianzisha mradi wa ujenzi wa nyumba 36 za watendaji wa CCM katika Mkoa wa Tanga, wenye thamani ya Shilingi bilioni tatu, ambapo hadi sasa tayari Shilingi bilioni 1.5 zimepatikana na ujenzi unaendelea katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Akizungumza mbele ya mlezi wa CCM Mkoa wa Tanga, Rabia Abdallah Hamid, mwenyekiti huyo amesema kuwa katika awamu ya kwanza na ya pili alitoa Shilingi milioni 500 kwa kila awamu, huku awamu ya tatu akipata Shilingi milioni 500 nyingine zilizolenga kuendeleza ujenzi huo.

Amesema fedha hizo zimefanya jumla ya mchango wake kufikia Shilingi bilioni 1.5 kati ya Shilingi bilioni tatu zinazohitajika kukamilisha mradi huo.
“Nilipoeleza kuwa ninakuja kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga na kuhakikisha najenga nyumba 36 katika mkoa huu, wengi hawakuamini, lakini nilikuwa na dhamira ya kweli ya kuhakikisha jambo hilo linatekelezwa,” amesema Abdurahmani.
Aidha, amesema uwepo wa mlezi wa mkoa huyo umempa nafasi ya kumkabidhi Shilingi milioni 500 zilizopatikana katika awamu ya tatu ili aweze kujionea maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo.

Katika hatua nyingine, Abdurahmani amesema Mkoa wa Tanga umeanza maandalizi ya kuadhimisha miaka 50 ya kuzaliwa kwa CCM, itakayofanyika Februari 5, 2027, kwa kutekeleza miradi mbalimbali yenye kulenga kuimarisha shughuli za chama na kuchangia maendeleo ya wananchi.
Amesema kuwa katika kuadhimisha miaka hiyo, ameamua kuelekeza nguvu pia katika kuwawezesha wakulima kwa kutafuta matrekta 40 yatakayosaidia shughuli za kilimo katika wilaya za mkoa huo.
Kwa mujibu wa Abdurahmani, matrekta hayo yanatarajiwa kugawanywa kwa wilaya, kila wilaya ikipata matrekta matano, yatakayotumika kutoa huduma za kulima mashamba kwa wakulima kwa gharama ya nusu ya bei ya kawaida.

Ameeleza kuwa mkulima anayelipa Shilingi 60,000 kwa hekta moja atalipia Shilingi 30,000 kupitia mpango huo, hatua ambayo amesema inalenga kupunguza gharama za uzalishaji na kuwawezesha wakulima kuongeza tija katika shughuli zao.
Amesema mpango huo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais na Mwenyekiti wa CCM katika kuwawezesha wakulima kupitia ruzuku ya mbolea na hatua nyingine za kuboresha sekta ya kilimo.
Akihitimisha hotuba yake, Abdurahmani amemuomba mlezi wa CCM Mkoa wa Tanga kufikisha salamu kwa Katibu Mkuu wa CCM na kumweleza azma ya mkoa huo, huku akimkaribisha atakapopata nafasi kuja kuzindua rasmi mpango wa matrekta kabla ya kuanza kusambazwa katika wilaya husika.

No comments:
Post a Comment