KAPINGA : VIWANDA VYA TANZANIA KULENGA UCHUMI WA DOLA TRILIONI MOJA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, November 2, 2026

KAPINGA : VIWANDA VYA TANZANIA KULENGA UCHUMI WA DOLA TRILIONI MOJA



Na Boniphace Epimack,OKULYBLOG – Dodoma


Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amesema mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Sekta ya Viwanda na Biashara nchini yametokana na maelekezo na miongozo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, yanayolenga kuimarisha uchumi wa Taifa kupitia uzalishaji na biashara.

Waziri Kapinga ameyasema hayo leo, Novemba 2, 2026, jijini Dodoma wakati akifungua rasmi maonesho maalumu yanayoambatana na maandalizi ya uzinduzi wa sera mbili muhimu za Taifa, ambazo ni Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya Mwaka 2025 na Sera ya Maendeleo ya Biashara Ndogo na za Kati ya Mwaka 2003, Toleo la 2025.

Amesema uzinduzi rasmi wa sera hizo utafanyika Jumatano, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.

Ameeleza kuwa mapitio ya sera hizo yamefanyika ili kuendana na kasi ya maendeleo ya Serikali ya Awamu ya Sita pamoja na maono ya Rais Samia ya kuifikisha Tanzania katika uchumi wa Dola Trilioni moja ifikapo mwaka 2050.

“Tunafahamu katika Dira ya Maendeleo ya 2050, Sekta ya Viwanda inategemewa kuchangia asilimia 15 ya Pato la Taifa na kukua kwa takribani asilimia tisa kila mwaka. Ndiyo maana tulikubaliana lazima tufanye mapitio ya sera hizi ili ziendane na kasi ya uchumi tunaoutamani,” amesisitiza Kapinga.

Katika hatua nyingine, Waziri Kapinga ametoa maelekezo kwa taasisi zilizo chini ya Wizara yake, akiwataka kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu yao ili kukuza viwanda, biashara na ujasiriamali nchini.

Akiwaelekeza Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), amelitaka kuendelea kuwaunga mkono wajasiriamali wadogo, hususan vijana, kwa kuwajengea uwezo na kuboresha ubora na mwonekano wa bidhaa zao ili ziweze kushindana katika masoko.

“Bidhaa za wajasiriamali wetu ni nzuri sana, ukigusa unaweza usiamini kama ni za Tanzania. Wengi ni vijana wadogo wamejiongeza. Changamoto iliyobaki ni umaliziaji wa bidhaa (finishing) na ufungashaji (packaging). SIDO hakikisheni mnaendelea kuwashirikisha na kuwasaidia,” amesema.

Aidha, ameitaka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuharakisha utoaji wa ithibati za ubora wa bidhaa, huku Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) ikiagizwa kuendelea kufungua fursa za masoko ya nje kupitia kampeni ya Made in Tanzania, kwa lengo la kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi na kukuza mapato ya Taifa.

Kwa upande wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Waziri Kapinga amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha wafanyabiashara wengi zaidi wanarasimisha shughuli zao ili kupunguza biashara zisizo katika mfumo rasmi.

Katika tukio hilo, Waziri Kapinga pia ametoa nasaha kwa wanafunzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) waliohudhuria maonesho hayo, akiwahimiza kuzingatia masomo, kuepuka vishawishi na kutumia elimu kama msingi wa kufikia malengo yao ya maisha.

“Elimu ndiyo kila kitu kwenye maisha yetu. Mkae shuleni, someni, epukeni vishawishi. Sisi kama wazazi tunawekeza sana kwenye elimu yenu. Go make your parents proud,” amewasihi wanafunzi hao, huku akiwataka kutumia fursa ya maonesho hayo kujifunza masuala mbalimbali ya ujasiriamali na biashara.

Maonesho hayo yanayofanyika jijini Dodoma yamewakutanisha wawakilishi wa viwanda vikubwa, wajasiriamali wadogo, taasisi za Serikali, wasanii pamoja na vikundi mbalimbali vya hamasa.

Maonesho hayo yataendelea leo na kesho, ambapo wananchi wa Dodoma na maeneo jirani wamekaribishwa kutembelea mabanda mbalimbali ili kujionea bidhaa zinazozalishwa nchini na kujifunza fursa zilizopo katika Sekta ya Viwanda na Biashara.









No comments:

Post a Comment