Na Boniphace Epimack -OKULY BLOG, DODOMA
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Denis Londo, amesema Tanzania haina budi kuachana na uchumi wa kuuza malighafi nje na badala yake kujikita katika kuongeza thamani ya rasilimali zake kama njia pekee ya kufikia uchumi wa Dola Trilioni 1 ifikapo mwaka 2050.
Mhe. Londo ameyasema hayo leo Novemba 3,2026 jijini Dodoma wakati akifungua Kongamano la Maendeleo ya Viwanda na kuzindua rasmi Programu ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Viwanda (PCP) kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) kwa kipindi cha 2026 hadi 2031.
Akimnukuu mwanafalsafa Fanon, Londo amesema kizazi cha sasa kina jukumu la kihistoria ambalo hakiwezi kukwepa.
"Every generation has its historical responsibility... Kila kizazi kina jukumu lake la kihistoria, kinapaswa kugundua jukumu hilo, na aidha kulisaliti au kulitekeleza," alisema Londo. "Wazee wetu kama Kanali Makalia na Prof. Chigunda waliweka msingi. Sisi tuna bahati ya kuandika Dira ya 2050 na wakati huo huo kushiriki katika kuitekeleza."
Naibu Waziri huyo amesema kuwa nadharia ya soko huria duniani inabomoka, ambapo mataifa makubwa sasa yanatumia ushuru na rasilimali kama maji na madini kama silaha za kisiasa na kiuchumi.
"Zamani ushuru ulitumika kulinda viwanda vya ndani, sasa unatumika kama silaha ya kuzuia wengine wasifike walipofika wengine. Maji sasa si usalama au uvuvi tu, maji ni silaha," alisema, akieleza kuwa ndio maana bei za bidhaa duniani zinapanda na kuathiri hata Watanzania.
amesema ndio maana umuhimu wa Muungano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar unazidi kuwa mkubwa katika kutumia uchumi wa buluu (Blue Economy) kama nguzo ya viwanda.
Londo amesema PCP iliyozinduliwa leo inaakisi moja kwa moja Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo msingi wake mkuu ni mageuzi ya vijijini (Rural Transformation).
"Hatuzungumzii kuongeza idadi ya viwanda tu, tunazungumzia kuzalisha tija, ajira na ustawi wa wananchi vijijini ambako Watanzania wengi wanaishi," alisisitiza.
Mhe. Londo amesema kuwa Sheria ya Fedha ya mwaka 2026/2027 imeelekeza asilimia 5 ya mapato yote ya ndani ya halmashauri nchini kuelekezwa kujenga miundombinu ya uzalishaji ikiwemo maeneo ya uwekezaji na kongani za viwanda, pamoja na asilimia 10 ya awali kwa makundi ya wanawake, vijana na walemavu.
amesema Wizara kupitia SIDO na TAMISEMI itahakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa.
Aidha, amekumbusha kuwa utekelezaji wa Dira ya 2050 unategemea asilimia 70 ya nguvu ya sekta binafsi, lakini akataka kujifunza kutokana na makosa ya ubinafsishaji wa viwanda vya zamani.
"Tunajua tulipokosea tulipobinafsisha viwanda vyetu. Kongamano hili lijadili ni aina gani ya sekta binafsi tunayoitaka ishiriki kutimiza Dira ya 2050," alisema.
Pia ame zitajaa miradi ya kimkakati ya Mchuchuma, Liganga na Magadi Soda ya Engaruka kama msingi wa kupunguza gharama za uzalishaji wa chuma, mashine za kilimo na vifaa vya ujenzi nchini.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Balozi Waziri Salum, amesema kongamano hilo limeandaliwa mahususi kujadili fursa, changamoto na hatua za kuongeza uwekezaji, uzalishaji na uongezaji thamani ya malighafi za ndani.
"Jukumu la kongamano hili ni kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050," alisema Balozi Salum.
Amefafanua kuwa kupitia PCP, Serikali inatarajia kuimarisha uratibu wa miradi ya viwanda, kukuza ujuzi, kuvutia uwekezaji, kuongeza mauzo ya nje na kuendeleza uzalishaji unaozingatia utunzaji wa mazingira , Programu hiyo itatekelezwa kwa pamoja Tanzania Bara na Zanzibar kwa kuunganisha rasilimali, teknolojia na uwekezaji kutoka kwa wadau mbalimbali.
Balozi Salum aliongeza kuwa Wizara itahakikisha maoni na mapendekezo yote yatakayotolewa na wadau katika kongamano hilo yanafanyiwa kazi kwa kushirikiana na taasisi husika ili kuhakikisha kongamano linaleta matokeo ya kweli kwa maendeleo ya viwanda nchini.









No comments:
Post a Comment