SERIKALI YAIMARISHA MIUNDOMBINU YA SAYANSI, YASISITIZA UWEKEZAJI KATIKA TEKNOLOJIA NA UBUNIFU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, November 3, 2026

SERIKALI YAIMARISHA MIUNDOMBINU YA SAYANSI, YASISITIZA UWEKEZAJI KATIKA TEKNOLOJIA NA UBUNIFU

 

Na. Erick Nenda- OKULY BLOG, DODOMA


Serikali imeendelea kuimarisha uwekezaji katika sekta ya sayansi, teknolojia na ubunifu kupitia ujenzi wa miundombinu ya taasisi za kisayansi, ikiwemo jengo la Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), lililowekewa jiwe la msingi jijini Dodoma.



Akizungumza katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la jengo hilo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema uwekezaji huo unahakisi kipaumbele cha Serikali katika kuendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu kama nguzo muhimu za maendeleo ya taifa.

Amesema dhamira hiyo inaonekana pia katika hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali, ikiwemo kutenga fedha za maendeleo kwa ajili ya sayansi na teknolojia, kujenga shule za sekondari za wasichana za sayansi katika mikoa mbalimbali pamoja na kupanua fursa za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wenye ufaulu wa juu katika masomo ya sayansi.


“Kuonyesha kipaumbele ambacho Rais wetu amekiweka katika masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu. Kipaumbele hiki tunakiona kwa kuelimisha fedha za maendeleo, lakini tunaona vilevile katika shughuli nyingine zote ambazo amezitengeneza,” amesema Profesa Mkenda.


Ameeleza kuwa Serikali imeimarisha mpango wa Samia Scholarship STEM kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo ya sayansi kidato cha sita, ili kuwawezesha kuendelea na masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati katika vyuo vikuu vya ndani ya nchi.


Aidha, amesema Serikali imepanua ufadhili huo kupitia Samia Scholarship Extended, inayowawezesha Watanzania kuendelea na masomo ya juu katika maeneo ya kimkakati ikiwemo sayansi ya nyuklia, sayansi ya takwimu (Data Science) na akili unde (Artificial Intelligence).


Akizungumzia sayansi ya nyuklia, Profesa Mkenda amesema eneo hilo lina matumizi mapana katika sekta za afya, kilimo na mazingira, hivyo ni muhimu kwa Tanzania kuandaa wataalamu wenye ujuzi wa kutosha.


“Sayansi ya nyuklia siyo mabomu pekee. Kuna afya, kuna kilimo, kuna mazingira na masuala mengine chungu nzima ambayo yanahitaji wataalamu,” amesema mkenda.


Amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika sayansi na teknolojia kwa kuhakikisha kuwa wanafunzi, wahadhiri na watafiti wanapata mazingira na fursa zinazowawezesha kufanya tafiti zenye matokeo na kushiriki katika maendeleo ya teknolojia duniani.


Uwekaji wa jiwe la msingi la jengo la COSTECH ni sehemu ya uwekezaji wa miundombinu ya taasisi za sayansi na teknolojia jijini Dodoma, huku Serikali ikiendelea kuimarisha mazingira ya utafiti, uvumbuzi na uzalishaji wa maarifa nchini.










No comments:

Post a Comment