
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi, ametumia salamu zake kwa wananchi wa Kibiti kutoa msukumo wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akitaka ahadi ya shilingi milioni 500 za kushughulikia upungufu wa maji ifuatiliwe, huku akionya kuwa watakaochezea fedha za wananchi watachukuliwa hatua.
Makamu wa Rais amesema maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha fedha zinazotolewa zinawahudumia wananchi, na kwamba wasaidizi wake wana wajibu wa kusimamia matokeo.
“ Mhe. Rais Hataki kuona fedha ya umma inachezewa,” amesema, akisisitiza kuwa Serikali haitamvumilia mzembe wala mtu atakayezichukulia fedha za maendeleo ya Kibiti kuwa mali yake.
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso kuwa Kibiti mjini inakabiliwa na upungufu wa maji wa takribani lita milioni 1.8 kwa siku, na kuahidi Wizara yake kuleta timu ya wataalamu na shilingi milioni 500 kuanza kazi ya kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo.
Aweso ameeleza kuwa vyanzo mbadala vilivyotambuliwa ni pamoja na visima virefu katika maeneo ya Kitembo na Mkupuka.
Makamu wa Rais ametaka kufikishiwa taarifa ya utekelezaji wa ahadi hiyo, kuthibitisha kufika kwa timu na hatua zilizochukuliwa, ili amfikishie Rais taarifa ya utekelezaji.
Kauli hiyo imeweka suala la maji katika ufuatiliaji wa moja kwa moja wa uongozi wa juu, baada ya Mbunge wa Kibiti Mhe. Amina Mkumba kueleza kuwa licha ya miradi iliyotekelezwa, wananchi bado wanahitaji suluhisho la kudumu la maji safi na salama.
Mbunge huyo pia ameomba Kibiti ijumuishwe katika manufaa ya mradi mkubwa wa maji kutoka Mto Rufiji unaotarajiwa kuhudumia Dar es Salaam na maeneo ya Pwani.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amekemea vikali migogoro ya wakulima na wafugaji inayoendelea maeneo mengi ya mikoa ya kusini, na kumtaka Mkuu wa Mkoa wa Pwani kusimamia sheria na kuchukua hatua dhidi ya yeyote anayechangia kuhatarisha usalama wa wananchi kwa masilahi binafsi.
Amesema uhamaji wa mifugo lazima ufuate taratibu, akionya dhidi ya kuingiza mifugo kwenye maeneo ya watu kwa njia za rushwa au makubaliano yanayopuuza matumizi halali ya ardhi.
“Tusioneane haya,” amesema, akisisitiza kuwa hatua zichukuliwe bila kujali cheo cha anayehusika.
Kuhusu ombi la stendi ya kisasa, Makamu wa Rais amewataka viongozi wa Kibiti kuandaa pendekezo la mradi lenye mahitaji, gharama na manufaa yanayotarajiwa, kisha waliwasilishe Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI.
Amesema Serikali ina utaratibu wa kufadhili miradi ya kimkakati katika Halmashauri, lakini viongozi wa eneo husika wanapaswa kuwasilisha mipango inayoeleza namna miradi hiyo itakavyohudumia wananchi na kuongeza mapato.
Kwa viongozi, ujumbe wa Makamu wa Rais umekuwa wazi,fedha za maendeleo lazima zionekane katika huduma wanazopata wananchi.
Makamu wa Rais amehitimisha ziara yake ya kikazi ya Mikoa ya Kusini na Pwani iliyofanyika kwa siku saba, akianzia Ruvuma, Mtwara, Lindi na kuhitimisha Pwani.




No comments:
Post a Comment