Na Mwandishi Wetu - Dar es salaam
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amesema Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini (TIMC) unaotajwa kuwa MGODINI KUMEITIKA unatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kukuza uwekezaji, kuongeza ujuzi na kuibua fursa mpya zitakazochochea ukuaji wa uchumi wa viwanda nchini.
Dkt. Kiruswa amesema, mpaka sasa zaidi ya wageni 1,500 kutoka ndani na nje ya nchi tayari wamethibitisha kushiriki mkutano huo, hatua inayoonesha kuongezeka kwa mvuto wa Tanzania katika uwekezaji wa sekta ya madini.
Hayo yamebainishwa leo Novemba 15, 2026, wakati akizungumza katika kipindi cha 360 kinachorushwa mubashara na vituo vya Clouds TV na Clouds FM.
Dkt. Kiruswa ameeleza kuwa, mkutano huo utatoa fursa kwa wadau wa sekta ya madini kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya sekta hiyo, yakiwemo uongezaji thamani madini, utoaji wa huduma migodini na ushirikishwaji wa wananchi katika uchumi wa madini.
Akizungumzia kuhusu uongezaji thamani madini, Dkt. Kiruswa amefafanua kuwa, Serikali imeweka kipaumbele katika kuhakikisha madini yanayozalishwa nchini yanaongezwa thamani kabla ya kufikishwa katika masoko, hatua inayolenga kuongeza mapato, ajira na manufaa ya kiuchumi kwa Watanzania.
Ameongeza kuwa, Tanzania imepiga hatua kubwa katika eneo hilo, ikiwemo kuanzishwa kwa viwanda zaidi ya saba vya kusafisha dhahabu vinavyoweza kufisha kwa kiwango cha asilimia 99.999.
Aidha, ameongeza kuwa, Serikali inaendelea kuimarisha maendeleo ya madini mkakati pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa katika utafiti na uchimbaji ili kuongeza uzalishaji na kubaini maeneo mapya yenye rasilimali za madini.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa ameeleza kuwa Wizara ya Madini inaendelea kusimamia utoaji wa leseni mbalimbali zinazowezesha shughuli za madini nchini, zikiwemo leseni za biashara ya madini kwa wafanyabiashara wakubwa na madalali, leseni za uchimbaji mdogo, wa kati na mkubwa.
Amewahimiza wananchi na wadau mbalimbali kushiriki na kufuatilia Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini 2026 ili kupata elimu, kutambua fursa zilizopo na kujifunza namna bora ya kunufaika na rasilimali za madini.
Akielezea kuhusu Program ya madini kwa kesho iliyo njema (MBT), Dkt. Kiruswa amewataka vijana kutumia fursa ya mkutano huo ili kupata taarifa mbalimbali za uwekezaji katika sekta ya madini hususan katika mnyororo mzima wa thamani madini ili kuingia katika mnyororo huo.
Sambamba na hilo, ametoa onyo kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya utoroshaji wa madini, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi na udhibiti wa shughuli za madini na kuwachukulia hatua za kisheria wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.
Mkutano wa TIMC 2026 unabebwa na kaulimbiu inayosema Uongezaji thamani madini ni chachu ya kukuza uchumi na maendeleo ya viwanda.




No comments:
Post a Comment