MAKAMU WA RAIS AKEMEA MIGOGORO YA ARDHI RUFIJI, ATAKA VIONGOZI WAWAJIBIKE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, November 16, 2026

MAKAMU WA RAIS AKEMEA MIGOGORO YA ARDHI RUFIJI, ATAKA VIONGOZI WAWAJIBIKE


Na Mwandishi Wetu - Ikwiriri, RUFIJI


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi ameagiza viongozi mkoani Pwani kuchukua hatua dhidi ya wanaochochea migogoro ya wakulima na wafugaji, akisisitiza kuwa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan haitakubali wananchi kuendelea kuumizwa huku wenye dhamana wakishindwa kuwajibika.
Akizungumza na wananchi wa Ikwiriri, wilayani Rufiji, wakati akitokea ziara ya kikazi mikoa ya Kusini, Makamu wa Rais amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe.Stanslaus Nyongo na Kamati ya Ulinzi na Usalama kusimamia utatuzi wa migogoro hiyo na kuwawajibisha wanaokiuka taratibu za kuingiza mifugo katika maeneo ya wananchi.
 
Amesisitiza kuwa viongozi hawapaswi kusubiri Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu wafike ndipo wachukue hatua. Aidha, ametaka maamuzi kuhusu ugawaji na matumizi ya ardhi yashirikishe wananchi, huku akihimiza haki, kuheshimiana na umoja wa Watanzania bila kujali makabila yao.
 
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mbunge wa Jimbo la Rufiji, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ameipongeza Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji katika elimu, afya na miundombinu, huku akimweleza Makamu wa Rais vipaumbele vya wananchi, ikiwemo kuharakisha ujenzi wa barabara ya Nyamwage - Utete, kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji na kuimarisha upatikanaji wa umeme na gesi ili kuchochea uwekezaji wa viwanda na kuongeza ajira.
 
Katika kusukuma maendeleo ya Rufiji, Makamu wa Rais amesema Serikali itaharakisha kuanza kwa mradi wa mabwawa mawili na miundombinu ya kuzuia mafuriko. Amesema mradi huo una umuhimu katika kukuza kilimo na kupunguza madhara ya mafuriko ya Mto Rufiji.
 
Kuhusu kilio cha wananchi cha barabara, umeme na gesi, Makamu wa Rais amewataka viongozi wa Wizara husika kutoa majibu mbele ya wananchi. Majibu hayo yameeleza mipango ya kuendeleza barabara ya Nyamwage - Utete, kuimarisha umeme kwa laini kutoka Mkuranga na kuwezesha upatikanaji wa gesi viwandani kupitia taratibu za uwekezaji.
 
Kwa wakulima wa korosho, amesisitiza kuwa salfa itaendelea kutolewa kwa ruzuku ya Serikali, huku changamoto za ubora wake zikifuatiliwa. Amewahimiza kuendelea na uzalishaji, akieleza kuwa wasaidizi wa Rais watasimamia utekelezaji wa maelekezo ya kuwafikishia pembejeo bora kwa wakati.
 
Akihitimisha, Makamu wa Rais ametoa onyo kali kwa wanaotaka kugeuza fedha za miradi ya wananchi kuwa njia ya kujitajirisha, akisisitiza uwajibikaji na hatua dhidi ya rushwa.

No comments:

Post a Comment