TAMWA-ZNZ YAANZA MCHAKATO WA KUTHIBITISHA SERA YA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI NA FARAGHA. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, November 16, 2026

TAMWA-ZNZ YAANZA MCHAKATO WA KUTHIBITISHA SERA YA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI NA FARAGHA.


Na Berema Suleiman Zanzibar.


Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania kwabupamde wa Zanzibar (TAMWA-ZNZ) kimeanza mchakato wa kuthibitisha Sera ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na Faragha (Data Protection and Privacy Policy) kupitia mkutano wa mashauriano na wadau uliofanyika Novemba 13, 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mifumo ya taasisi katika kuhakikisha taarifa binafsi zinakusanywa, zinachakatwa, zinahifadhiwa na kutumiwa kwa kuzingatia misingi ya usalama, usiri na faragha.

Sera hiyo inalenga kuweka mwongozo rasmi wa namna ya kusimamia na kulinda taarifa zinazopatikana katika utekelezaji wa shughuli za TAMWA-ZNZ, zikiwemo taarifa za wafanyakazi, wanufaika wa miradi, washirika na wadau.

Aidha, itaweka utaratibu wa uwajibikaji katika matumizi na usambazaji wa taarifa hizo ili kuzuia uvujaji, matumizi yasiyoidhinishwa na ukiukwaji wa haki za faragha za wamiliki wa taarifa.


Akielezea sababu za kuandaa sera hiyo, Sabrina Mwintanga, Afisa Programu kutoka TAMWA-ZNZ, alisema Sabrina Yussuf Mwintanga alisema hatua hiyo imetokana na dhamira ya taasisi kuimarisha mifumo yake ya kiutendaji kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo inayosimamia ulinzi wa taarifa binafsi.

Alisema katika utekelezaji wa programu na miradi yake, TAMWA-ZNZ hukusanya taarifa za makundi mbalimbali katika jamii, hivyo ni muhimu kuwa na mwongozo unaoelekeza namna taarifa hizo zinavyopaswa kushughulikiwa katika kila hatua.

“Tumeliona suala la ulinzi wa taarifa binafsi kuwa muhimu kutokana na aina ya shughuli tunazozitekeleza na makundi mbalimbali tunayofanya nayo kazi. 

Ni wajibu wetu kuhakikisha taarifa tunazokusanya zinalindwa na kutumiwa kwa madhumuni yaliyokusudiwa. 

Sera hii itatuwezesha kuwa na utaratibu ulio wazi wa ukusanyaji, uhifadhi, matumizi na ushirikishwaji wa taarifa hizo kwa kuzingatia usiri, usalama na haki za wamiliki wa taarifa,” amesema Sabrina.

Ameongeza kuwa sera hiyo itasaidia kujenga utamaduni wa uwajibikaji miongoni mwa wafanyakazi na kuimarisha uaminifu kati ya taasisi na wadau wake, hususan makundi yaliyo katika mazingira hatarishi, yakiwemo wanawake, watoto, manusura wa ukatili wa kijinsia na watu wenye ulemavu.

Kwa upande wake, Hijja Shamte Abdalla, Afisa Uhusiano na Utetezi kutoka Shirika la Jumuiya za Watu wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA), alisema uwepo wa sera hiyo ni muhimu katika kulinda haki, utu na faragha za watu wenye ulemavu, ambao taarifa zao binafsi hukusanywa na taasisi mbalimbali wakati wa utekelezaji wa programu za maendeleo.

Amesisitiza kuwa umuhimu wa kuhakikisha taarifa hizo zinashughulikiwa kwa usiri na usalama ili kuepusha matumizi au usambazaji unaoweza kuhatarisha haki na usalama wao.

Naye Hassan Saidi Salum kutoka Mwavuli wa Asasi za Kiraia Zanzibar ANGOZA alisema taarifa binafsi ni rasilimali yenye thamani inayopaswa kulindwa, hivyo uwepo wa sera hiyo utaiwezesha TAMWA-ZNZ kuimarisha mifumo yake ya ndani, kuongeza uwajibikaji na kujenga imani kwa watu na taasisi zinazoshirikiana nayo.


Akichangia katika mkutano huo, Salum Suleiman Ali, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na mwakilishi katika masuala ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na Faragha, alisema ulinzi wa taarifa unapaswa kuzingatiwa katika shughuli zote za taasisi, ikiwemo matumizi ya mifumo ya kiteknolojia, usimamizi wa nyaraka na mahusiano ya kikazi.

Ameeleza kuwa taarifa binafsi zinahitaji kulindwa katika mzunguko wake wote, kuanzia ukusanyaji, uchakataji na matumizi hadi uhifadhi, ushirikishwaji au uondoaji wake kwa mujibu wa taratibu husika. 

Ameongeza kuwa mkutano huo ni sehemu ya hatua ya uthibitishaji wa wadau (Stakeholders Validation), inayolenga kupata maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuhakikisha rasimu ya sera inakidhi mahitaji ya kiutendaji na kuzingatia misingi ya kisheria.

Mkutano huo uliwakutanisha wadau kutoka taasisi mbalimbali, zikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Zanzibar University (ZU), Jukwaa la Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, Zanzibar (THRDC), SHIJUWAZA, ANGOZA, ZYF, PYI, TAMWA-ZNZ Pamoja na wadau wengine.

Tanzania ina Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2022 (Personal Data Protection Act, 2022), Na. 11 ya mwaka 2022, iliyotungwa kwa lengo la kulinda haki ya faragha ya watu binafsi kwa kuweka utaratibu wa kisheria unaosimamia ukusanyaji, uchakataji, matumizi na uhifadhi wa taarifa binafsi. 

Sheria hiyo pia ilianzisha Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (Personal Data Protection Commission – PDPC) kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wake. Sheria hiyo ilianza kutumika rasmi Mei 1, 2023, na juhudi za TAMWA-ZNZ kuandaa sera yake ya ndani ni sehemu ya kuimarisha mifumo ya taasisi katika kuzingatia matakwa ya kisheria na kuhakikisha taarifa za wafanyakazi, wanufaika na wadau wake zinalindwa dhidi ya matumizi yasiyoidhinishwa na ukiukwaji wa faragha.

No comments:

Post a Comment