Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi, ameendeleza ziara yake ya kikazi mkoani Lindi kwa kutembelea Jimbo la Mchinga na kugawa mitungi ya gesi kwa wananchi wa Kijiji cha Kilangala, akisisitiza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia ni hatua muhimu katika kulinda afya, kutunza mazingira na kupunguza gharama za maisha.
Katika hafla hiyo, Makamu wa Rais amesema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi kupitia huduma bora na utekelezaji wa miradi.
Amesema ugawaji wa mitungi hiyo una umuhimu unaogusa maisha ya kila siku ya familia, hasa kwa kupunguza matumizi ya kuni na mkaa pamoja na madhara ya moshi unaotokana na upishi.
“Tunachokifanya hapa leo ni kitu kikubwa sana,” amesema Makamu wa Rais, akiwahimiza wananchi kutumia nishati safi ya kupikia kwa manufaa ya afya zao na mazingira.
Shughuli hiyo pia imekuwa nafasi ya kuzipatia majibu hoja za wananchi zilizowasilishwa na Mbunge wa Jimbo la Mchinga Mhe. Salma Kikwete kuhusu maji, umeme, barabara, afya, umwagiliaji na miundombinu ya uvuvi.
Makamu wa Rais amempongeza mbunge huyo kwa kuendelea kuwasemea wananchi wa Mchinga, huku akiwataka viongozi na watendaji walioambatana naye kueleza hatua za utekelezaji wa miradi katika maeneo yao.
Katika suala la maji, Wizara ya Maji imeeleza kuwa mradi wa Nangaru umefikia asilimia 80, huku mkandarasi na wahandisi wakielekezwa kukamilisha kazi ndani ya mwezi mmoja ili wananchi waanze kupata huduma ya maji safi na salama.
Kwa upande wa umwagiliaji, imeelezwa kuwa mradi wenye ukubwa wa hekta 800 na thamani ya shilingi bilioni 71 unatarajiwa kuanza kutekelezwa baada ya kupatikana kwa fedha za malipo ya awali kwa mkandarasi.
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bw. Raymond Mndolwa amesema mradi huo utaanza utekelezaji mwaka huu baada ya kupokea mgao wa fedha unaotarajiwa mwishoni mwa Novemba mwaka huu.
Katika sekta ya afya, TAMISEMI imeeleza kuwa zaidi ya shilingi milioni 600 zimepelekwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Kituo cha Afya cha Nang’ao. Aidha, utekelezaji wa barabara unaendelea kwa awamu, pamoja na mipango ya kuweka taa katika barabara iliyozungumziwa kwenye mkutano huo.
Wananchi wa Mchinga pia wameelezwa kuhusu mpango wa kujenga soko la samaki, mwalo na miundombinu ya kuhifadhia samaki, wenye fedha za shilingi bilioni 1.06. Utekelezaji wake unatarajiwa kuanza kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Kuhusu nishati ya umeme, Makamu wa Rais amesema Serikali inaendelea na hatua za kuongeza uwezo wa transfoma ili kukabiliana na mahitaji yanayoongezeka, sambamba na utekelezaji wa mradi wa kuunganisha mikoa ya Lindi na Mtwara kwenye Gridi ya Taifa.
Amesisitiza kuwa uwekezaji huo unalenga kuwawezesha wananchi kupata umeme wa uhakika kwa matumizi ya nyumbani na shughuli za uzalishaji.
Akihitimisha hotuba yake kabla ya kukabidhi mitungi ya gesi kwa wananchi, Makamu wa Rais amewashukuru wananchi wa Mchinga kwa kujitokeza kwa wingi, akisema Serikali itaendelea kusikiliza mahitaji yao na kuyafanyia kazi.






No comments:
Post a Comment