REA YATINGA 16 BORA MPIRA WA WAVU SHIMMUTA 2026 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, November 13, 2026

REA YATINGA 16 BORA MPIRA WA WAVU SHIMMUTA 2026


Na Mwandishi Wetu, Morogoro


TIMU ya mpira wa wavu ya wanaume ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imefanikiwa kutinga hatua ya 16 bora ya michuano ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania (SHIMMUTA) mwaka 2026 inayoendelea mkoani Morogoro.

REA imekata tiketi hiyo licha ya kupoteza mchezo wake wa mwisho kwa seti 2–0 (25–12, 25–8) mbele ya mabingwa watetezi wa mwaka 2025, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST). Hata hivyo, ushindi na pointi ilizokusanya katika michezo ya awali zimeipa REA wastani mzuri uliotosha kuivusha hatua ya makundi.

Akizungumza na wanahabari mara baada ya mchezo huo,usiku wa tarehe 12 Novemba, 2026, mshambuliaji tegemeo wa REA na Nahodha, Mhandisi, Samson Kanoth, amesema kikosi chao kimesahau matokeo hayo na sasa kinaelekeza nguvu zote kwenye michezo ya mtoano.

“Hatua ya 16 bora ni ngumu sana kwa sababu ukifungwa unaaga mashindano. Tunafahamu kuwa kila timu iliyofika hatua hii ni bora, lakini sisi tumejipanga kikamilifu kukabiliana na mpinzani yeyote tutakayepangwa naye,” amesema Mhandisi Kanoth.

Michuano ya SHIMMUTA kwa mwaka huu inaendelea kushika kasi mkoani Morogoro ikishirikisha taasisi na mashirika mbalimbali nchini kwa lengo la kuimarisha afya na ushirikiano mahali pa kazi.

No comments:

Post a Comment