RUJAT YAONGEZA WANACHAMA KWA ASILIMIA 155 NDANI YA MIAKA MINNE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, November 3, 2026

RUJAT YAONGEZA WANACHAMA KWA ASILIMIA 155 NDANI YA MIAKA MINNE



NA SHUA NDEREKA, OKULY BLOG


Chama cha Waandishi wa Habari za Vijijini Tanzania (RUJAT) kimepiga hatua kubwa katika kupanua wigo wa wanachama wake baada ya kuongeza idadi kutoka 47 mwaka 2022 hadi kufikia wanachama 120 mwaka 2026, sawa na ukuaji wa asilimia 155 ndani ya kipindi cha miaka minne.

Mafanikio hayo yanaashiria kuongezeka kwa mwitikio na imani ya waandishi wa habari kwa chama hicho, ambacho kimeendelea kujenga mtandao wa waandishi wanaojihusisha na habari za vijijini.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu na mafanikio ya chama kwa kipindi cha mwaka 2023 hadi 2026, katika Kongamano la Mwaka la Tathmini ya Huduma za Habari na Mawasiliano Vijijini nchini Tanzania, lililoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Vijijini Tanzania (RUJAT), jijini Dodoma, Katibu wa chama cha RUJAT Prosper Kwigize, amesema ongezeko hilo ni sawa na wanachama wapya takribani 73 ikilinganishwa na idadi iliyokuwepo mwaka 2022.

Amesema hatua hiyo si mwisho wa safari ya ukuaji wa RUJAT, kwani tayari kuna maombi mapya kutoka kwa waandishi wa habari 62 wanaotamani kujiunga na chama hicho, hali inayoonesha fursa kubwa iliyopo ya kuendelea kupanua mtandao wake na kuwafikia waandishi wengi zaidi.

Ameeleza kuwa ukuaji huo ni hatua muhimu katika kuimarisha uwakilishi wa chama, kuongeza nguvu ya pamoja ya wanachama na kupanua wigo wa utekelezaji wa shughuli zake katika maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, katika kipindi cha mwaka 2023 hadi 2026, RUJAT imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuimarisha mifumo ya uongozi na utawala, kupanua wigo wa ushirikiano na taasisi za serikali na wadau wa maendeleo, kuongeza idadi ya wanachama, kushiriki katika majukwaa ya kitaifa na kimataifa, kuanzisha tovuti rasmi ya chama, pamoja na kutafuta fursa za rasilimali kwa ajili ya kuendeleza shughuli zake.

Akizungumzia mchango wa utekelezaji wa majukumu hayo katika ukuaji wa chama, Kwigize amesema, mafanikio yaliyopatikana yamechangia kuimarisha uwajibikaji, ushirikishwaji wa viongozi katika maamuzi na uendelevu wa shughuli za RUJAT.

Pia, miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyopatikana ni RUJAT kujitambulisha kwa serikali na taasisi mbalimbali za umma, ikiwemo Ofisi ya Rais, Ikulu, pamoja na wizara na sekta mbalimbali, hatua iliyoongeza mwonekano wa chama na kutoa fursa ya kujenga uelewa kuhusu nafasi ya waandishi wa habari za vijijini katika kuwasilisha changamoto, fursa na maendeleo ya wananchi.

“Kujitambulisha kwa taasisi za serikali ni hatua muhimu katika safari ya RUJAT ya kujenga uaminifu, kuimarisha mahusiano ya kitaasisi na kutafuta fursa za kushirikiana katika miradi na programu zenye manufaa kwa wananchi”. Amesema Kwigize

Kwigize amesema chama hicho kimepiga hatua katika kujitambulisha na kujenga mahusiano kwenye majukwaa ya kimataifa na kikanda yanayohusiana na habari, maendeleo ya vyombo vya habari na ushirikiano wa kitaasisi.

Amesema, miongoni mwa taasisi na majukwaa ambayo chama kimefanikiwa kujitambulisha au kuhusiana nayo ni DW (Deutsche Welle)-mtandao wa kimataifa wa utangazaji, RFI (Radio France Internationale)- mtandao wa kimataifa wa utangazaji, UNESCO- Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, MiCT- taasisi inayohusiana na maendeleo ya vyombo vya habari na mawasiliano; pamoja na majukwaa ya wahariri wa Afrika Mashariki, Asia na Ulaya.

“Mahusiano hayo yameongeza fursa kwa RUJAT kuonekana katika mazingira mapana ya tasnia ya habari, kujifunza kutoka kwa wadau wengine na kutafuta nafasi za ushirikiano wa kitaalamu”.

Kwa ujumla, mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka 2023 hadi 2026 yamekuwa muhimu katika safari ya maendeleo ya Chama cha Waandishi wa Habari za Vijijini Tanzania (RUJAT) na yanapaswa kuwa msingi wa hatua kubwa zaidi katika kipindi kijacho, huku chama kikiendelea kuimarisha utawala wake, kuongeza uwezo wa wanachama na wigo wa miradi.

No comments:

Post a Comment