SEKTA YA NISHATI KUCHOCHEA UWEKEZAJI NA UKUAJI WA VIWANDA NCHINI – DKT. HOMERA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, November 3, 2026

SEKTA YA NISHATI KUCHOCHEA UWEKEZAJI NA UKUAJI WA VIWANDA NCHINI – DKT. HOMERA



Abu Dhabi, UAE


Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amesema Tanzania inaendelea kujipanga kimkakati kuitumia sekta ya nishati kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi, kuongeza ushindani wa ukuaji wa viwanda na kuvutia uwekezaji, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mageuzi ya kiuchumi nchini.

Dkt. Homera ameyasema hayo wakati akizungumza katika kikao cha Mawaziri wa Nishati kilichofanyika wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Nishati (ADIPEC 2026), unaofanyika Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Amesema Serikali inalenga kuibadilisha sekta ya nishati kutoka katika utoaji wa huduma za kawaida za umeme na gesi na kuifanya kuwa nyenzo muhimu ya kimkakati katika kukuza uzalishaji wa viwanda, ikiwemo viwanda vya mbolea, kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza mvuto wa Tanzania kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Akizungumzia hatua zilizofikiwa katika kuongeza uzalishaji wa umeme, Dkt. Homera amesema kukamilika kwa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa kuzalisha MW 2,115 kumeongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini kufikia MW 4,646, ikilinganishwa na mahitaji ya juu ya MW 2,271.

Amesema hali hiyo imeiwezesha Tanzania kuwa na ziada ya umeme wa MW 2,375, hatua inayofungua fursa zaidi za uwekezaji katika viwanda vinavyohitaji matumizi makubwa ya umeme.

Aidha, ameongezea kuwa Serikali inaendelea kupanua miundombinu ya usafirishaji umeme ya msongo wa kilovoti 400 (400kV) ili kuimarisha upatikanaji wa nishati ya uhakika katika maeneo ya shughuli za uchimbaji madini na miundombinu mikubwa ya kimkakati, ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR).

Akielezea malengo ya muda mrefu ya Serikali, Dkt. Homera amesema Tanzania inalenga kuongeza uwezo wa uzalishaji umeme kufikia MW 8,000 ifikapo mwaka 2030 na MW 15,000 ifikapo mwaka 2031, huku ikilenga kuhakikisha asilimia 75 ya umeme unaozalishwa unatokana na vyanzo safi vya nishati, ikiwemo gesi asilia na maji.

Amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika vyanzo vya nishati jadidifu ili kuongeza wigo wa uzalishaji na kuimarisha usalama wa nishati nchini. Miradi hiyo ni pamoja na Mradi wa Umeme wa Jua Kishapu wenye uwezo wa MW 100, pamoja na miradi ya umeme wa upepo inayopangwa kutekelezwa katika maeneo ya Manyoni na Nzega.

Vilevile, amesema Tanzania inaendelea na mipango ya kuendeleza miradi ya jotoardhi yenye lengo la kufikia MW 5,000, ambapo MW 30 zinatarajiwa kuanza kuzalishwa mwaka wa fedha 2026/27 na kuongeza uwezo huo kufikia MW 130 ifikapo mwaka 2030.

Amesisitiza kuwa uwekezaji katika vyanzo mbalimbali vya nishati na upanuzi wa miundombinu yake ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha nishati ya uhakika, nafuu na endelevu inapatikana kwa ajili ya kuchochea shughuli za uzalishaji, ukuaji wa viwanda na maendeleo ya uchumi wa Taifa.

ADIPEC ni mkutano na maonesho ya kimataifa ya nishati ambapo mwaka huu imezikutanisha nchi zaidi ya 30, makampuni zaidi ya 2,250 ambapo viongozi wa nishati wanajadili mambo mbalimbali ikiwemo uhakika na usalama wa nishati haswa kutokana na athari za kisiasa mashariki ya kati, pia matumizi ya akili Unde (AI) katika sekta ya nishati ni mada kuu zinazotawala jukwaa hilo.





No comments:

Post a Comment