Shamba Janja (Smart Farm) limezinduliwa tarehe 9 Novemba 2026 katika Chuo cha Kilimo cha Mt. Maria Gorethi, mkoani Iringa, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Climate Smart Agriculture (CSA - CoVE), unaolenga kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika kilimo.
Shamba hilo limeanzishwa kuwa kituo cha mafunzo kwa vitendo na matumizi ya teknolojia zinazolenga kuongeza tija, kupunguza gharama za uzalishaji na kuimarisha uwezo wa sekta ya kilimo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza katika uzinduzi huo kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa NACTVET, Meneja wa Mipango na Ufuatiliaji, Bw. Justine Kaiza, amesema Shamba Janja ni hatua muhimu katika kuimarisha elimu na mafunzo ya ufundi stadi yanayozingatia teknolojia, ubunifu na mahitaji ya sekta ya kilimo.
Amesema kupitia shamba hilo, wanafunzi, wakufunzi na wakulima watapata fursa ya kujifunza matumizi ya mifumo ya umwagiliaji yenye ufanisi, vihisi vya unyevunyevu wa udongo, ufuatiliaji wa hali ya hewa na usimamizi wa mazao kwa kutumia taarifa sahihi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Profyta, Bw. Ewout Schurink, amesema teknolojia hizo zitasaidia wakulima kuongeza uzalishaji na kipato huku wakipunguza gharama kwa kutumia maji, mbolea na kemikali kwa ufanisi zaidi.
Aidha, zinamwezesha mkulima kufuatilia na kusimamia shughuli za shamba akiwa mbali na eneo la uzalishaji.
Uzinduzi huo umehusisha wadau 165 wa kilimo, wakiwemo wanafunzi, wakulima, wakufunzi, Maafisa kilimo na wadau wengine wa sekta hiyo.
Kwa upande wa mafunzo, Shamba Janja linatarajiwa kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na kuwajengea uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa katika sekta ya kilimo. Pia, litatoa fursa kwa wakulima kujifunza na kutumia teknolojia hizo katika shughuli zao za uzalishaji.
NACTVET itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha teknolojia na maarifa yanayopatikana kupitia mradi huu yanatumika na kuendelezwa katika vyuo vinavyonufaika, pamoja na kupanua matumizi yake katika vyuo vingine vya kilimo.
Mradi wa CSA-CoVE unalenga kuimarisha elimu na mafunzo ya kilimo yanayozingatia teknolojia, kuongeza fursa za ajira na ujasiriamali kwa vijana, na kujenga sekta ya kilimo yenye tija na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Mradi wa CSA-CoVE unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya na kutekelezwa kwa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Maastricht cha nchini Uholanzi, Shule ya American farm ya nchini Ugiriki, Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Taasisi ya Kilimo Profyta, Chuo cha Kilimo cha Mt. Maria Goreth, Chuo cha Kilimo na Mifugo Kilacha, Chuo cha Kilimo MATI Mlingano, na Kituo cha Mafunzo ya Kilimo cha Kilimanjaro (KATC).




No comments:
Post a Comment