TANZANIA KUENDELEZA USHIRIKIANO NA SHIRIKA LA MAENDELEO LA UFARANSA (AFD) - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, November 13, 2026

TANZANIA KUENDELEZA USHIRIKIANO NA SHIRIKA LA MAENDELEO LA UFARANSA (AFD)

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El- Maamry Mwamba, akiagana na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Bi. Sandra Kassab, baada ya Mkutano wao kuhusu ushirikiano wa maendeleo, uliofanyika katika Ofisi ya Katibu Mkuu, Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El- Maamry Mwamba akiteta jambo na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Bi. Sandra Kassab, baada ya Mkutano wao kuhusu ushirikiano wa maendeleo, uliofanyika katika Ofisi ya Katibu Mkuu, Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El- Maamry Mwamba akieleza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), wakati wa Mkutano na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Bi. Sandra Kassab, uliofanyika katika Ofisi ya Katibu Mkuu, Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Idara ya Afrika wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Bi. Sandra Kassab, akieleza nia ya Shirika hilo kuendelea kufadhili miradi ya maendeleo, wakati wa Mkutano na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El- Maamry Mwamba, uliofanyika katika Ofisi ya Katibu Mkuu, Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El- Maamry Mwamba, akimkabidhi zawadi Mkurugenzi wa Idara ya Afrika wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Bi. Sandra Kassab baada ya kumalizika mkutano wao kuhushu ushirikiano wa Maendeleo, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.
Ujumbe wa Wizara ya Fedha ukiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El- Maamry Mwamba, wakati wa Mkutano na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Bi. Sandra Kassab baada ya kumalizika mkutano wao kuhushu ushirikiano wa Maendeleo, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.
Ujumbe ulioambatana na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Bi. Sandra Kassab, ukifuatilia mkutano kati ya Mkurungenzi huyo na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El- Maamry Mwamba, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El- Maamry Mwamba, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Bi. Sandra Kassab (wa nne kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka Wizara ya Fedha na AFD, baada ya kumalizika kwa mkutano kati yao, uliofanyika katika Ofisi ya Katibu Mkuu, Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El- Maamry Mwamba, akimuongoza mgeni wake Mkurugenzi wa Idara ya Afrika wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Bi. Sandra Kassab, walipomaliza mkutano wao kuhusu ushirikiano wa maendeleo, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.



(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Dar es Salaam)


Na. Peter Haule, WF, Dar es Salaam.


Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa maendeleo na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kufadhili miradi ya kimkakati inayolenga kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El- Maamry Mwamba, alipokutana na kufanya mazungunzo na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika wa AFD, Bi. Sandra Kassab, jijini Dar es Salaam.

Dkt. Mwamba amesema Tanzania inathamini ushirikiano wa muda mrefu na Serikali ya Ufaransa kupitia AFD, ulioanza miaka ya 1970, ambapo moja ya miradi ya awali iliyofadhiliwa na Serikali hiyo ilikuwa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam mwaka 1979, huku ushirikiano na AFD ukiimarika zaidi kuanzia miaka ya 1990.

“AFD imeendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo kwa kufadhili miradi katika sekta za nishati, maji na usafi wa mazingira, miundombinu ya usafiri, kilimo, umeme vijijini, misitu na uhifadhi wa mazingira”, amesema Dkt. Mwamba

Amebainisha kuwa kwa sasa AFD ina miradi 12 inayoendelea nchini yenye thamani ya Euro bilioni 1.13, huku Euro milioni 175 zikiwa tayari zimeidhinishwa kwa ajili ya miradi mitatu inayohusiana na maji na usafi wa mazingira pamoja na mabadiliko ya tabianchi.

Katika kuendeleza ushirikiano huo, Dkt. Mwamba amesema Serikali inatarajia kushirikiana na AFD kupata ufadhili wa miradi mingine iliyo kwenye hatua za maandalizi, ikiwemo miradi ya Nishati Mseto wa Mafia, mipango ya Uchumi wa Buluu, Mradi wa Kuunganisha Gridi za Umeme za Uganda na Tanzania, Mradi wa Taifa wa Maendeleo ya Kidijitali pamoja na mkopo usio wa Serikali kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).

Aidha, ametoa rai kwa AFD kuendelea kudumisha kiwango cha ufadhili kwa miradi ya maendeleo nchini licha ya kukamilika kwa programu za Extended Credit Facility (ECF) na Resilience and Sustainability Facility (RSF) za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) mwezi Julai 2026.

Aidha, Dkt. Mwamba amesisitiza umuhimu wa kujenga uwezo wa makandarasi wazawa wa kazi za ujenzi ili waweze kushindana kikamilifu na wakandarasi wa kigeni katika utekelezaji wa miradi ya kitaifa.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza ushiriki wa kampuni za ndani na kuhakikisha manufaa zaidi ya kiuchumi yanayotokana na miradi hiyo yanabaki nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika wa AFD, Bi. Sandra Kassab, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za maendeleo, Serikali ya Tanzania na sekta binafsi ili kuvutia uwekezaji kutoka Ulaya, hususan Ufaransa, kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya viwanda na kukuza uchumi wa Tanzania.

Amesema ushirikiano huo unaweza kusaidia kampuni za Ulaya kutambua fursa zilizopo nchini, kutoa suluhisho za kiteknolojia na kiufundi pamoja na kujenga ubia wa muda mrefu unaolenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumzia masuala ya ununuzi katika miradi mbalimbali, Bi. Kassab amesisitiza umuhimu wa kuzingatia miongozo ya ununuzi ili kuhakikisha kuwa zabuni zinapotangazwa kunakuwa na wigo mpana wa uchaguzi na ushindani, utakaowezesha kupatikana kwa huduma na bidhaa zenye ubora kwa bei zinazostahili.

Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakuwa na ubora na uwezo wa kudumu kwa muda mrefu.

Ameongeza kuwa uwekezaji haupaswi kuishia katika uuzaji wa vifaa au utekelezaji wa miradi pekee, bali unapaswa kujumuisha pia huduma za uendeshaji, matengenezo na usaidizi wa kitaalamu wa muda mrefu ili kuhakikisha miradi inakuwa endelevu na inatoa huduma bora kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment