Ikulu, Dar es Salaam.
Waziri wa Nishati Mhe. Juma Zuberi Homera ameeleza kwamba Tanzania imepata ahadi mbalimbali za uwekezaji, ufadhili na ushirikiano wa kiufundi katika Sekta ya Nishati kufuatia ushiriki wake katika Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31) unaoendelea jijini Antalya, Uturuki.
Ahadi hizo zinatarajiwa kuimarisha juhudi za Serikali katika kuendeleza nishati jadidifu na nishati safi ya kupikia.
Ameeleza hayo wakati wa mkutano na waandishi wa Habari uliofanyika leo Novemba 15, 2026 Ikulu, jijini Dar es Salaam ambao ulikuwa ukitoa taarifa ya ziara ya Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Uturuki ambapo alishiriki mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31).
Mhe. Dkt Homera ameeleza kwamba miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni ahadi ya Serikali ya Saudi Arabia kuendelea kufadhili miradi ya nishati ikiwemo nishati jadidifu na nishati safi ya kupikia. Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nayo imeidhinisha ufadhili wa majiko ya umeme 70,000 huku majiko mengine 70,000 yakitarajiwa kuidhinishwa hivi karibuni.
Aidha, taasisi ya SEforALL imeahidi kushirikisha sekta binafsi kuunda muungano wa wawekezaji kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji katika sekta hiyo na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa teknolojia za nishati safi ya kupikia.
Kwa upande wake, International Solar Alliance (ISA) imeahidi kushirikiana na Tanzania kuhamasisha matumizi ya nishati ya jua katika shule na vituo vya afya pamoja na kutenga dola za Marekani milioni 200 kwa ajili ya miradi ya umeme jua katika nchi wanachama.
Mashirika mengine yaliyotoa ahadi za ushirikiano ni pamoja na Shirika la Kimataifa la Nishati Jadidifu (IRENA), Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), UK Aid na Serikali ya Iceland. UK Aid imeahidi kutoa pauni milioni 4 kwa ajili ya miradi ya nishati safi ya kupikia na nishati jadidifu pamoja na kuwezesha upatikanaji wa majiko ya umeme kwa wananchi kupitia mfumo wa malipo kidogo kidogo.
Wizara ya Nishati imeeleza kuwa hatua inayofuata ni kuendelea na mazungumzo na wadau walioahidi ushirikiano huo ili kuhakikisha ahadi hizo zinageuzwa kuwa miradi ya maendeleo itakayochangia upatikanaji wa nishati ya uhakika, nafuu na endelevu kwa wananchi.
Wakati huo huo, Serikali imeendelea kuonesha mafanikio katika Sekta ya Nishati ambapo kiwango cha upatikanaji wa umeme nchini kimeongezeka kutoka asilimia 78.4 mwaka 2020 hadi asilimia 85.5. Vilevile, idadi ya taasisi zinazotumia nishati safi ya kupikia imefikia 2,745, na idadi ya mitungi 370,792 na majiko banifu 139,859 imegawiwa kwa wannanchi.




No comments:
Post a Comment