Timu ya soka ya Tume ya Madini imeendeleza wimbi la ushindi katika Mashindano ya SHIMMUTA baada ya kuifunga timu ya Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) kwa bao 1–0 katika mchezo uliofanyika leo, Novemba 11, 2026, kwenye Uwanja wa Morogoro Sekondari.
Mchezo huo ulioshuhudia ushindani mkubwa ulizikutanisha timu mbili zilizokuwa na dhamira ya kupata ushindi. Hata hivyo, Tume ya Madini ilitumia vyema nafasi iliyoipata na kufanikiwa kufunga bao pekee lililoamua matokeo ya mchezo huo.
Katika mchezo huo, safu ya ulinzi ya Tume ya Madini, ikiongozwa na nahodha Shabani Mtambo, ilionesha uimara na nidhamu ya hali ya juu kwa kuzuia mashambulizi ya wapinzani na kuhakikisha lango la timu hiyo linabaki salama hadi mwisho wa mchezo.
Ushindi huo umeongeza alama muhimu kwa Tume ya Madini na kuimarisha morali ya wachezaji wanapojiandaa kwa michezo mingine ya mashindano hayo.
Katika mchezo mwingine, timu ya wanawake ya Tume ya Madini ya mchezo wa kuvuta kamba nayo imeendeleza mafanikio baada ya kuifunga timu ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa ushindi wa 2–0, na hivyo kuonesha ushindani na uwezo wa Tume ya Madini katika michezo mbalimbali.
Timu ya soka ya Tume ya Madini inatarajiwa kurejea dimbani kesho, Alhamisi, Novemba 12, 2026, kukabiliana na timu ya Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MNUAT), katika mchezo mwingine wa kuwania ushindi kwenye mashindano hayo.







No comments:
Post a Comment