WAZIRI MAVUNDE AWATAKA WENYE VIWANDA VYA KUONGEZA THAMANI MADINI KUWA SOKO LA MADINI YA WACHIMBAJI WADOGO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, November 3, 2026

WAZIRI MAVUNDE AWATAKA WENYE VIWANDA VYA KUONGEZA THAMANI MADINI KUWA SOKO LA MADINI YA WACHIMBAJI WADOGO


Na Mwandishi Wetu - Dodoma


Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amewataka wamiliki wa viwanda vya uongezaji thamani madini ya metali nchini kuwa soko la uhakika la madini yanayozalishwa na wachimbaji wadogo ili kuimarisha mnyororo wa thamani wa madini, kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi wa Taifa.

Mhe. Mavunde ametoa wito huo leo, Oktoba 3, 2026, wakati wa kikao chake na wamiliki wa viwanda hivyo katika Ofisi za Tume ya Madini jijini Dodoma Waziri ambapo amesisitiza umuhimu wa wamiliki wa viwanda kuingia katika makubaliano ya kibiashara yenye tija na wachimbaji wadogo, ili kuhakikisha wachimbaji wanapata soko la uhakika la madini yao na viwanda vinapata malighafi zinazohitajika kwa ajili ya uzalishaji.

Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuimarisha mnyororo wa thamani wa madini ya metali nchini, kuongeza uzalishaji na kuhakikisha manufaa ya uwekezaji katika viwanda vya uongezaji thamani yanawafikia pia wachimbaji wadogo.

Waziri Mavunde amepongeza muitikio wa Watanzania katika kuanzisha viwanda vya uongezaji thamani madini, akieleza kuwa uamuzi wa Serikali kuzuia usafirishaji wa madini ghafi ambayo hayajachakatwa nje ya nchi umechochea uwekezaji mkubwa katika sekta hiyo.

Amesema uwekezaji huo umewezesha kujifunza na kutumia teknolojia mpya, kuongeza ajira kwa Watanzania na kukuza mapato ya Serikali, sambamba na kujenga msingi wa uchumi unaotegemea uzalishaji wa bidhaa zenye thamani kubwa.

Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini, akieleza kuwa hatua zinazochukuliwa na Serikali zimekuwa chachu ya ukuaji wa sekta ya madini na kuvutia uwekezaji katika shughuli za uchakataji na uongezaji thamani.

“Ni jukumu la Serikali kuhakikisha wawekezaji hawa hawakwami. Wizara ya Madini itaendelea kutoa miongozo na ushirikiano unaohitajika ili kuhakikisha viwanda hivi vinafikia malengo ya kuanzishwa kwake,” amesema Mhe. Mavunde.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde amemuagiza Kamishna wa Madini na Tume ya Madini kutembelea viwanda vya Zamahero na Haneti vilivyoanza uzalishaji wa madini ya nikeli na shaba ili kubaini changamoto na kuwasilisha mapendekezo ya kuboresha mazingira ya uzalishaji.

Amesisitiza umuhimu wa wamiliki wa viwanda na wachimbaji wadogo kuweka makubaliano madhubuti ya kibiashara, akibainisha kuwa changamoto ya baadhi ya wachimbaji kushindwa kuwasilisha madini baada ya kupokea fedha za awali imeathiri uaminifu na upatikanaji wa malighafi na kwamba Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji ili kuhakikisha viwanda vinafanya kazi kwa tija, kuongeza ajira na kukuza matumizi ya teknolojia mpya.

Kwa upande wao, Wamiliki wa viwanda wameishukuru Serikali kwa kutatua changamoto ya muda mrefu ya umeme katika maeneo ya uzalishaji, huku Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini ya Metali Tanzania (TBMA), Tobias Kente, akimshukuru Waziri Mavunde kwa kuendelea kushughulikia changamoto za wadau wa sekta hiyo.

No comments:

Post a Comment