WAZIRI MKUU AITAKA NFRA KUHARAKISHA MAUZO YA MAZAO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, November 5, 2026

WAZIRI MKUU AITAKA NFRA KUHARAKISHA MAUZO YA MAZAO


WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba ameitaka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuharakisha taratibu za kuuza mazao pindi masoko yanapopatikana, ili kuepuka kupoteza fursa hizo kutokana na michakato mirefu.

Vilevile, amezitaka taasisi zinazohusika kuendelea kutafuta masoko ya kudumu na kuwezesha uuzaji wa mazao nje ya nchi, huku akieleza kuwa bei ya kununua mahindi kupitia NFRA imeongezwa kutoka shilingi 450 hadi shilingi 500.

Amesema hayo Bungeni, jijini Dodoma leo (Alhamisi, Novemba 05, 2026), wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, katika Mkutano wa Tano, Kikao cha Nane cha Bunge la 13.

Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Kongwa, Isaya Mngurumi Moses, aliyetaka kufahamu mikakati ya Serikali ya kutafuta masoko na kuboresha bei za mazao ili wakulima wanufaike na uzalishaji wao.

Dkt. Mwigulu amesema NFRA inapopata masoko inapaswa kukamilisha taratibu za mauzo kwa wakati, kwa sababu ucheleweshaji unaweza kuwafanya wanunuzi kupata mazao katika masoko mengine yenye michakato mifupi zaidi.

Amesema Serikali imekuwa ikitumia mazungumzo na viongozi wa mataifa mbalimbali kutafuta masoko ya mazao ya Tanzania na kupanua wigo wa biashara kwa wakulima.

Kuhusu bei ya mahindi, Waziri Mkuu amesema amekutana na Wizara yenye dhamana ya kilimo mara kadhaa kujadili namna ya kuboresha bei ya ununuzi kupitia NFRA.

Amesema bei hiyo iliongezwa kutoka shilingi 200 hadi shilingi 300, baadaye shilingi 450 na sasa shilingi 500.

“Tulikaa tena kwa mara ya mwisho, tukashauriana kwamba kama bado wanaweza kwenda juu zaidi, wafanye hivyo, na tulikubaliana sasa watapeleka iwe shilingi 500,” amesema.

Amewataka wakulima wenye mahindi wanayohitaji kuuza kufika katika ofisi za NFRA za mikoa na kanda ili kutumia fursa ya bei hiyo iliyoboreshwa.

Hata hivyo, amesema NFRA huenda isiweze kununua mahindi yote, hivyo jitihada za kupanua masoko na kuwezesha mauzo nje ya nchi zinapaswa kuendelea.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewaelekeza Wakuu wa Mikoa kuchukua hatua kali dhidi ya watu wanaopeleka mifugo katika mashamba ya wakulima bila ridhaa yao, akisisitiza kuwa Serikali haitakubali uvunjaji wa sheria wa makusudi.

Akijibu swali la Mbunge wa Nachingwea, Fadhili Ally Liwaka, kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji, amesema hatua zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya mtu aliyefanya kosa, bila kugeuza tukio hilo kuwa mgogoro kati ya jamii.

“Kama mmoja amefanya kosa hilo, achukuliwe hatua kali huyo huyo. Wala wakulima wasione wafugaji ni adui zao, na wala wafugaji wasione wakulima ni adui zao,” amesema.

Amewataka wananchi kuepuka kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutumia vyombo vya sheria kutafuta haki.

Vilevile, amewaelekeza viongozi katika ngazi mbalimbali kuimarisha mipango ya matumizi bora ya ardhi na kusitisha ugawaji wa maeneo kinyemela. Amesema rushwa, matumizi mabaya ya ofisi na ugawaji wa ardhi usiofuata taratibu vinachochea migogoro katika jamii.

Kuhusu huduma za afya, Waziri Mkuu amesema Serikali itafanya uandikishaji wa awamu ya pili wa bima ya afya kwa wote ili kuendelea kuyafikia makundi ambayo bado hayajafikiwa.

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Stella Alex Ikupa, kuhusu matibabu kwa watu wenye ulemavu ambao bado hawajafikiwa na mpango huo, amezitaka taasisi za afya kuendelea kuwahudumia kupitia dirisha la msamaha wa matibabu.

“Pasitokee mtu kukosa matibabu kwa sababu ya hali yake ya ulemavu ama hali yake ya kifedha,” amesema.

Amewahimiza pia Watanzania kuendelea kujisajili katika mfumo wa bima ya afya kwa wote, akisisitiza kuwa mpango huo unalenga wananchi wote, wenye kipato na wasio na kipato.

No comments:

Post a Comment