BoT YASISITIZA USIMAMIZI MADHUBUTI WA SEKTA YA FEDHA KULINDA AMANA ZA WANANCHI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, November 5, 2026

BoT YASISITIZA USIMAMIZI MADHUBUTI WA SEKTA YA FEDHA KULINDA AMANA ZA WANANCHI



Mkaguzi Mwandamizi wa Benki kutoka BoT, Bw. Joel Charles,akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu usimamizi wa sekta ya fedha yaliyoandaliwa na BoT, Novemba 5, 2026 jijini Dar es Salaam.


Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DAR ES SALAAM


Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti wa sekta ya fedha nchini kwa lengo la kulinda amana za wananchi, kuimarisha mifumo ya malipo na kuhakikisha taasisi za fedha zinafanya shughuli zake kwa usalama na ufanisi.

Akizungumza katika mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu usimamizi wa sekta ya fedha yaliyoandaliwa na BoT, Novemba 5, 2026, jijini Dar es Salaam, Mkaguzi Mwandamizi wa Benki kutoka taasisi hiyo, Bw. Joel Charles, amesema usimamizi huo ni muhimu katika kudumisha utulivu wa sekta ya fedha na kulinda maslahi ya wateja.

Amesema Benki Kuu ina jukumu la kusimamia na kudhibiti shughuli za taasisi mbalimbali za kifedha, zikiwemo benki za biashara, taasisi za huduma ndogo za fedha, kampuni za mikopo ya nyumba na taasisi nyingine za kifedha, ili kuhakikisha zinafuata sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa.

Akifafanua umuhimu wa usimamizi huo, Charles amesema unalenga kuhakikisha wananchi wanaendelea kuwa na imani na taasisi za fedha pamoja na mifumo inayotumika katika kutoa huduma hizo.

“Usimamizi wa sekta ya fedha ni muhimu katika kulinda amana za wananchi, kuhakikisha mifumo ya malipo inakuwa salama na kuimarisha uwezo wa taasisi za fedha kuendelea kutoa huduma kwa ufanisi,” amesema Charles.

Ameeleza kuwa usimamizi huo unalenga pia kuzuia na kudhibiti vitendo vya uhalifu wa kifedha, ikiwemo utakatishaji wa fedha haramu, pamoja na kulinda mifumo ya malipo na rasilimali za taasisi za fedha dhidi ya vihatarishi vinavyoweza kuathiri shughuli zake.

Katika mafunzo hayo, Charles amefafanua umuhimu wa taasisi za fedha kuwa na mitaji inayokidhi viwango vilivyowekwa na mamlaka husika, akieleza kuwa matakwa hayo husaidia kuimarisha uwezo wa taasisi hizo kuhimili changamoto za kifedha na kuendelea kutoa huduma kwa wateja.

Amesema viwango vya mitaji hutofautiana kulingana na aina ya taasisi ya fedha na shughuli zinazofanywa, hatua inayosaidia kuhakikisha taasisi hizo zinakuwa na msingi imara wa kifedha katika kutekeleza majukumu yake.

Aidha, amewataka waandishi wa habari kuzingatia weledi na usahihi wanaporipoti masuala yanayohusu sekta ya fedha, akisisitiza kuwa taarifa zisizo sahihi zinaweza kusababisha taharuki kwa wananchi na kuathiri imani ya umma kwa benki na taasisi za kifedha.

Ameongeza kuwa vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kutoa elimu ya fedha kwa umma kwa kuwasilisha taarifa kwa lugha inayoeleweka, huku vikizingatia misingi ya kitaalamu ili kusaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi kuhusu huduma za kifedha.

Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Benki Kuu ya Tanzania za kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu masuala ya uchumi na fedha, ili kuongeza uelewa wao na kuboresha namna wanavyowasilisha taarifa zinazohusu sekta ya fedha kwa jamii.


No comments:

Post a Comment