
Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imeeleza hatua inazochukua kutekeleza maagizo ya Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi, kuhusu kuongeza fursa za ajira kwa vijana nchini.
Maagizo hayo yalitolewa hivi karibuni jijini Arusha wakati wa Mkutano wa Watendaji Wakuu wa Taasisi za Serikali, ambapo Makamu wa Rais alielekeza kila mkuu wa taasisi kuhakikisha anaweka mpango madhubuti wa kuongeza fursa za ajira kwa vijana.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu mchango wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika utekelezaji wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya Mwaka 2025 na Marejeo ya Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Mwaka 2003, Toleo la Mwaka 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB, Bw. Asangye Bangu, amesema zaidi ya vijana 3,000 wamepata fursa za ajira kupitia mfumo huo kwa kufanya kazi katika maghala mbalimbali nchini.
Bw. Bangu amesema Mfumo wa Stakabadhi za Ghala umeendelea kuwa kichocheo cha ajira kwa vijana, hususan katika shughuli za upokeaji, uhifadhi, upimaji na usimamizi wa bidhaa ghalani, hatua inayochangia kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi.
Aidha, amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la mwamko wa vijana kushiriki mafunzo yanayowawezesha kupata ujuzi wa kufanya kazi katika maghala yanayotumia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.
“Awali tulikuwa tunapata washiriki kati ya 15 hadi 20 katika mafunzo haya, lakini sasa idadi imeongezeka hadi kufikia vijana 150 wanaohudhuria mafunzo kwa wakati mmoja. Hii inaonesha namna vijana wanavyozidi kutambua fursa zilizopo katika Mfumo wa Stakabadhi za Ghala,” amesema Bw. Bangu.
Ameeleza kuwa WRRB itaendelea kuimarisha utoaji wa mafunzo na kuhamasisha vijana kuchangamkia fursa zinazotokana na kupanuka kwa matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika sekta mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuongeza ajira na kukuza uchumi wa wananchi.

No comments:
Post a Comment