
Ndugu zangu,
Nimeshuhudia
mechi ya usiku wa jana tulipokuwa tukiangamizwa na Algeria. Mpaka
naamua kuinuka kitini tulikuwa tumeshapigwa saba bila. Ukweli
tulizidiwa, na kuna wakati nilimuuliza aliyekaa karibu yangu kama Mbwana
Samatta yumo uwanjani au Kocha Mkwassa ameshamuweka benchi. Hapana,
nilijibiwa kuwa yumo uwanjani!
Naam, hata nyota wetu Mbwana Samatta jana alikuwa wa kumtafuta kwa kuvaa miwani ya macho. Hakuonekana.
Nilichokiona
kikubwa; Tanzania tunahitaji kuruhusu uraia pacha ili nasi tuweze
kuwaleta vijana wetu wa Kitanzania wanaocheza ughaibuni na waliochukua
uraia wa nchi hizo. Maana, kwa soka ya sasa, ni vigumu kwenda Kombe la
Dunia kwa kuwa kikosini na akina Samatta wawili na waliobaki ni wa
kutoka Ligi ya nyumbani.
Na hakika
matokeo ya leo yalikuwa ni ya ajabu pia. Sikufikiri kwa soka ile
tuliyocheza Dar tungekwenda Algeria kucheza ' mediocre football' na
kutoka na matokeo yale. Nilitarajia tufanye miujiza, maana soka inayo ya
kwake. Na Algeria wenzetu wamewahi kufanya miujiza dhidi ya taifa kubwa
kisoka la Ujerumani.
Ndio,
itakumbukwa Algeria iliwahi kufanya miujiza katika fainali za Kombe la
Dunia za mwaka 1982. Ni pale ilipowafunga Ujerumani kwa mabao 2-1 kwenye
mechi ya ufunguzi katika kundi lao. Walikuwa wachezaji nyota wa Algeria
kama vile Assad na Madjer walionyesha kandanda safi na la kuvutia.
Katika
pambano hilo kipa wa Ujerumani Schumacher alitoka uwanjani akiwa
ameinamisha kichwa. Maana alitamka kabla ya mechi, kuwa kama Algeria
watawafunga Wajerumani, basi atafanya operesheni ya kubadili sura yake!
Pamoja na
Algeria kuwafunga Wajerumani, njama zilifanyika kwa Ujerumani na
Austria katika kundi lao. Kwa namna moja au nyingine matokeo yalipangwa
ili Algeria isipate nafasi ya kusonga mbele. Ujerumani iliibuka mshindi
kwa bao 1-0 matokeo ambayo yalizifanya Ujerumani na Austria kusonga
mbele kwa pamoja kutoka kwenye kundi lao.
Jambo
hilo lilidhihirishwa mara tu baada ya Ujerumani kupachika bao lao. Mpira
ukaonekana 'kufa'. Wachezaji wa timu zote mbili walionekana kucheza
wakisubiri kipenga cha mwamuzi cha kumaliza mchezo. Hakika hii yaweza
kabisa kusemwa ni moja ya kashfa zilizopata kutokea katika historia ya
fainali za Kombe la Dunia.
Kikabaki
kimya hata baada ya matokeo hayo ya kushangaza. Hayakuandikwa mengi
kwenye kurasa za michezo za magazetini. Kwenye moja ya magazeti ya
Austria walitenga ukurasa mzima bila kuandika habari za mechi hiyo.
Walichofanya ni kuandika orodha ya wachezaji waliocheza pambano hilo kwa
pande zote mbili.
Kwa
mchezo ule uliokuwa na matokeo ya ajabu na kutatanisha baina ya
Ujerumani na Austria , Chama Cha Soka cha Algeria kiliitaka FIFA izitoe
Ujerumani na Austria katika ushiriki wao wa mashindano hayo. Jambo hilo
halikufanyika.
Maggid,(P.T)
No comments:
Post a Comment