TANNZANIA YAKWEA "JINO
MOJA" VIWANGO FIFA. TANZANIA imekwea kwa nafasi moja katika viwango vipya
vitolewavyo kila mwezi na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA huku Uganda
wakiendelea kuongoza kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Kwa orodha hiyo iliyotolewa leo
Tanzania ndio wanaoburuza mkia kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki wakishika
nafasi ya 53 kwa upande wa Afrika huku majirani zutu Uganda wakiwa nafasi ya 14
na duniani wa 68, Rwanda nafasi ya 23 duniani wa 96, Kenya nafasi ya 48 duniani
125 na Burundi nafasi ya 40 duniani 107.
Katika tano bora kwa upande wa Afrika, Ivory
Coast ndio wanaoongoza kwasasa wakishikilia nafasi ya 22 wakifuatiwa na Algeria
walioko nafasi ya 26, Ghana ni watatu wakiwa nafasi ya 30. CapeVerde wamekwea
tena na kuingia tano bora za Afrika kwa kushikilia nafasi ya 32 duniani
wakifuatiwa na Senegal walioko nafasi ya 39.
Kwa ujumla duniani orodha hiyo sasa inaongozwa
na Ubelgiji walioikwaa nafasi hiyo kutoka kwa Argentina ambao wameporomoka
mpaka nafasi ya tatu, mabingwa wa dunia Ujerumani wao wako nafasi ya pili,
Ureno nafasi ya nne na tano bora inakamilishwa na mabingwa Copa Amerika Chile.
MARCELO AWAPA MCHECHETO DUNGA NA
BENITEZ.
KOCHA wa timu ya taifa ya Brazil, Dunga na
meneja wa Real Madrid Rafael Benitez wameingia katika mchecheto juu ya afya ya
Marcelo baada ya kupata majeruhi ya msuli wa paja katika ushindi wa bao 1-0
iliyopata timu yake katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Paris
Saint-Germain juzi.
Beki huyo mwenye umri wa miaka 27 alitolewa
katikati ya kipindi cha kwanza katika mchezo huo uliofanyika katika Uwanja wa
Santiago Bernabeu. Sasa nyota huyo kuna hati hati ya kuukosa mchezo muhimu wa
clasico dhidi ya mahasimu wao Barcelona na ule wa timu yake ya taifa ya Brazil
wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Argentina utakaofanyika huko Buenos Aires.
Akihojiwa Benitez amesema Marcelo
amekuwa akicheza mechi nyingi na walifahamu lolote linaweza kutokea ingawa
walidhani anaweza kupata muda wa kutosha kufikia mapumziko ya kupisha mechi za
kimataifa.
Benitez aliendelea kudai kuwa beki
huyo aligundua tatizo lake mapema na kumtaarifu kabla ya kuamua kutoendelea na
mchezo, na kwasasa wanasubiria vipimo kuona ukubwa wa tatizo. Brazil itakwaana
na Argentina Novemba 12 kabla ya kuikaribisha Peru Novemba 17 huku ule mchezo
wa clasico ukitarajiwa kuchezwa Novemba 21.
VIDEO YA NGONO YAMTESA BENZEMA.
MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa
Ufaransa na klabu ya Real Madrid, Karim Benzema amewekwa rasmi chini ya
uchunguzi leo akihusishwa na tuhuma za kulaghai ili kupata pesa kutoka kwa
Mfaransa mwenzake Mathieu Valbuena wakitumia mkanda wa video wa ngono.
Taarifa ya waendesha mashitaka wa
Versailles imedai kuwa tuhuma hizo za kihalifu ambazo zinachunguzwa inaweza
kubeba adhabu ya miaka siyopungua mitano jela. Wakili wa Benzema, Sylvain
Cormier aliwaambia wanahabari baada ya kusikilizwa kwa shitaka hilo kuwa mteja
wake alikuwa hana hatia na hakuhusika kwa vyovyote vile na tukio hilo la
kihalifu. Kesi hiyo imeanza kuleta wasiwasi juu ya ushiriki wa mchezaji huyo
katika michuano ya Euro 2016 ambayo itafanyika nchini Ufaransa.
RAIS WA DORTMUND ATUPA TAULO KWA
KUINYOOSHEA MIKONO BAYERN.
OFISA mkuu wa Borussia Dortmund,
Hans-Joachim Watzke amedai klabu yao haiwezi kushindania taji la Bundesliga na
Bayern Munich. Dortmund imekuwa katika kiwango kizuri toka ujio wa meneja mpya
Thomas Tuchel wakishika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi huku wakipoteza
mchezo mmoja pekee katika mashindano yote msimu huu, ingawa mchezo huo ukiwa
ule waliotandikwa mabao 5-1 na Bayern.
Bayern kwasasa ndio wanaongoza ligi
wakitofautiana na Dortmund kwa alama tano na Watzke anaamini mbio za ubingwa
zimeshakwisha. Akihojiwa Watzke amesema haina maana yeyote kuzungumzia kuhusu
kuifukuzia Bayern kwani mpaka sasa wameshapoteza alama pekee na kama
wakiendelea hivyo wanaweza kuendelea kutanua pengo la alama hadi kufikia nane
kwa msimu wote.
Watzke aliendelea kudai kuwa
wanachoangalia wao kwasasa ni jinsi wanavyofanya kwani wameimarika sana toka
ujio wa kocha mpya. Dortmund watakuwa wenyeji wa Qabala katika mchezo wa Europa
League baadae leo kabla ya kurejea Jumapili hii katika Bundesliga kwa kukwaana
na mahasimu wao wa Ruhr Schalke.
ENRIQUE AKIRI PAMOJA NA KUMKUMBUKA
MESSI LAKINI KIKOSI CHAKE HAKIMTEGEMEI.
MENEJA wa Barcelona, Luis Enrique
amekiri kikosi chake kinamkumbuka Lionel Messi lakini anaamini kwa matokeo
ambayo wamekuwa wakipata kunaonyesha kabisa hawamtegemei mshambuliaji huyo wa
kimataifa wa Argentina.
Barcelona iliibuka na ushindi wa
mabao 3-0 dhidi ya BATE katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya uliochezwa jana
kwa mabao yaliyofungwa na Neymar na Luis Suarez aliyefunga mawili.
Klabu hiyo ya Catalan ndio
wanaongoza kundi E wakiwa na alama 10 katika michezo minne waliyocheza hivyo
kuwafanya kuihitaji alama moja pekee katika mchezo wao dhidi ya AS Roma Novemba
24 ili waweze kufuzu hatua ya timu 16 bora.
Messi aliumia goti Septemba 26 katika mchezo
wa La Liga dhidi ya Las Palmas lakini ukosekana kwake kumeonekana kutokuwa na
athari kubwa kwani mabingwa hao wa Hispania na Ulaya wamepoteza mechi moja
katia ya nane walizocheza.
Akihojiwa Enrique amesema ni kweli
wanamkumbuka Messi lakini timu hiyo hiyo siku zote imekuwa na rasilimali ndio
maana unaona wanaendelea kufanya vyema pamoja na kumkosa nyota wao.
WENGER AKIRI ARSENAL KUWA NA NAFASI
FINYU YA KUSONGA MBELE LIGI YA MABINGWA ULAYA.
MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger
amesema kikosi chake kina nafasi finyu ya kutinga hatua ya timu 16 bora katika
michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kugaragazwa kwa mabao 5-1 na Bayern
Munich juzi.
Kipigo hicho kinaiacha Arsenal mkiani mwa
kundi F wakiwa alama sita nyuma ya vinara Bayern Munich na Olympiakos
wanaoshika nafasi ya pili.
Arsenal sasa lazima wawafunge Dinamo
Zagreb na Olymipakos katika mechi zao mbili za mwisho huku wakiomba Bayern
waifunge Wagiriki hao katika mchezo wao. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo
Wenger amesema bado wana nafasi lakini wanatakiwa kutambua kuwa nafasi yenyewe
ni finyu.
Kocha huyo aliendelea kudai kuwa
pamoja na hayo bado wataendelea kupambana mpaka mwisho.
YAMTIMUA RAMSEY.
KLABU ya Queens Park Rangers-QPR
imemtimua meneja wake Chris Ramsey ikiwa imepita miezi michache toka achukue
mikoba ya kuinoa timu hiyo.
Ramsey mwenye umri wa miaka 53
ambaye alisaini mkataba wa miaka mitatu Mei mwaka huu baada ya kuitumikia timu
hiyo kama kocha wa muda, alitimuliwa baada ya kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Derby
Count juzi ambacho kimewaacha wakining’inia katika nafasi ya 13 katika msimamo
wa ligi.
Mkurugenzi wa michezo wa QPR Les
Ferdinand alithibitisha taarifa hizo akidai kuwa kile walichokuwa wakikitegemea
kutoka kwa kocha huyo hakukipata ndio maana wakaamua kuzitisha mkataba naye.
QPR waliteremka daraja kutoka Ligi
Kuu Mei baada ya Harry Redknapp kujiuzulu kama meneja Februari na Ramsey
kuchukua mikoba yake.
No comments:
Post a Comment