RAIS MAGUFULI KUIKOSA STARS NA ALGERIA KESHO, DK SAMIA SASA NDIYE MGENI RASMI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, November 14, 2015

RAIS MAGUFULI KUIKOSA STARS NA ALGERIA KESHO, DK SAMIA SASA NDIYE MGENI RASMI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli hataweza kuhudhuria mchezo wa soka kati ya Tanzania na Algeria kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

 
Badala yake, Makamu wa Rais, Dk. Samia Hassan Suluhu ndiye atakuwa mgeni rasmi katika mchezo huo wa kwanza Raundi ya Pili kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2018 Urusi.
 
Hiyo inafuatia Rais Magufuli kufiwa na mjukuu wake, Maryfaustna Mlyambina, aliyefariki Novemba 11, 2015 Kimara mjini Dar es Salaam na jana kusafirishwa mkoani Mwanza kwa mazishi. 
 
Lakini taarifa zinasema Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais Mstaafu, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete naye atakuwepo leo Uwanja wa Taifa kuongoza hamasa kwa wachezaji waifunge Algeria.
Rais Dk John Pombe Joseph Magufuli amefiwa na mjukuu wake, hivyo hatakuwepo Uwanja wa Taifa leo

Mchezo wa kesho utakuwa wa nane kihistoria kuzikutanisha timu hizo, Tanzania ikishinda mara moja, kutoa sare tatu na kufungwa tatu.
 
Taifa Stars iliifunga Algeria Januari 21 mwaka 1995 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zilizofanyika mwaka 1996 Afrika Kusini wakati marudiano Algeria ilishinda 2-1 Julai 28, mwaka 1995 mjini Algiers, hiyo ilikuwa hatua ya makundi ya mtoano.
 
Kabla ya hapo, timu hizo zilikutana mara ya kwanza kabisa katika Michezo ya Afrika (All Africans Games) mjini Lagos, Nigeria Januari 8, mwaka 1973 na  Algeria ikashinda 4-2.
 
Timu hizo zikaja kukutana tena katika mchezo wa michuano ya ufunguzi wa Uwanja wa Uhuru baada ya ukarabati, iliyopewa jina Kombe la Sumaye na Algeria ikashinda 1-0 Dar es Salaam Oktoba 4, mwaka 1997.
 
Timu hizo zikaja kukutana tena katika mechi ya kirafiki ya kimataifa Agosti 18 mwaka 2002 na kutoa sare ya bila kufungana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 
Zikakutana tena Septemba 3, mwaka 2010 kuwania tiketi ya Mataifa ya Afrika na kutoa sare ya 0-0 Algiers wakati marudiano Septemba 3 mwaka 2011, timu hizo zikatoa tena sare ya 1-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na huo ndiyo ulikuwa mchezo wa mwisho timu hizo kukutana.
 
Baada ya mchezo wa leo timu hizo zitarudiana mjini Algiers Jumanne na mshindi wa jumla atakwenda hatua ya makundi ambayo itakuwa ya mwisho ya mchujo katika mbio za Urusi 2018.

No comments:

Post a Comment