Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Maombezi (GRC) la Dar es Salaam, Anthony Lusekelo, maarufu Mzee wa Upako, amekamatwa na polisi akituhumiwa kumfanyia fujo na kutishia kumuua jirani yake.
Tukio
hilo lilitokea juzi maeneo ya Kawe wilayani Kinondoni, Dar es Salaam,
kuanzia saa 11 asubuhi hadi saa tatu alipochukuliwa na polisi wa Kituo
cha Kawe.
Wakati
wa tukio hilo, Mchungaji Lusekelo alikuwa ameegesha gari lake
barabarani kiasi cha kusababisha usumbufu na foleni ya magari mengine.
Chanzo
cha tukio hilo kinadaiwa ni kulipiza kisasi kwa jirani zake hao
wanaoishi katika nyumba namba KAW/MZN/1348, ambao alidai wamekuwa
wakimkebehi kuwa hafai kuwa mchungaji kwa sababu ya ulevi.
Licha
ya baadhi ya watu kumsihi aondoke eneo hilo kutokana na hadhi yake,
mchungaji huyo alikaidi, huku akiendelea kuongea kwa sauti iliyofanana
na mtu mwenye kilevi.
Baadhi ya maneno yaliyosikika kwenye video iliyorekodiwa eneo la tukio hayaandikiki kwa kuwa si ya kawaida.
“Mjinga wewe, mimi ni zaidi ya askari na wewe ni mgambo, na si mgambo wewe ni raia tu.
“Umenitukana
sana wewe mpaka leo nimeamua kuloana na mvua, usitoe gari hapo mshenzi
sana wewe, na nikikuona mahali popote…, mshenzi kabisa, muangalie sana
huyo,” alisikika Mchungaji Lusekelo akiongea kwa sauti.
Baada ya kuongea maneno hayo, ilisikika sauti ya mwanamke kutoka ndani ya uzio wa nyumba hiyo ikimjibu mchungaji huyo: “Huwezi, aniangalie kitu gani.”
Hata
hivyo, hata watu mbalimbali walipomsihi aache kutoa lugha hizo za
kejeli na aondoe gari lake lililokuwa limesababisha foleni, alikataa
akisema hataliondoa hadi atakapokuja Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro.
Baada
ya purukushani hizo, polisi kutoka katika Kituo cha Kawe walifika eneo
hilo saa tatu asubuhi, wakamchukua mchungaji huyo na kumpeleka kituoni.
Inadaiwa
baada ya kufikishwa kituoni hapo, mchungaji huyo alipimwa kiwango cha
ulevi na kukutwa 131, ambacho kinaelezwa kuwa ni kikubwa – ulevi wa
kupindukia.
Ilipofika
saa tano asubuhi, mchungaji huyo alihamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi
(Central), ambako huko nako inadaiwa alipimwa kilevi na kuonekana
kushuka hadi kufikia 121.
Alipotafutwa
Kamishna Sirro ili kuzungumzia sakata la mchungaji huyo, alisema
atalizungumzia leo katika mkutano wake na waandishi wa habari.
No comments:
Post a Comment