RAIS John Magufuli amefichua siri ya hatua yake ya kuitumbua Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Amesema
alilazimika kuchukua hatua hiyo baada ya bodi hiyo kuidhinisha Sh
bilioni 26 kupelekwa kuwekwa kwenye akaunti maalumu( Fixed Account)
katika benki kadhaa za biashara.
Bodi
hiyo ilitoa idhini ya kupelekwa fedha hizo katika benki hizo wakati
kuna agizo la Rais la kupiga marufuku kwa taasisi za umma, mashirika ya
umma, idara za serikali, wakala na wizara kuweka fedha zao katika benki
za kibiashara.
Fedha hizo zinatakiwa zifunguliwe akaunti katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Jumapili
iliyopita asubuhi, Ikulu ilitangaza kwamba Dk Magufuli ameivunja Bodi
ya Wakurugenzi ya TRA, na saa chache akateua Naibu Kamishna Mkuu mpya.
Ikulu
bila kueleza sababu, ilisema kwamba Rais Magufuli ametengua uteuzi wa
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRA, Bernard Mchomvu na kuivunja
bodi nzima.
Aidha,
pamoja na kuivunja bodi hiyo alimteua Charles Kichere kuwa Naibu
Kamishna Mkuu wa TRA, kuziba nafasi iliyokuwa wazi kwa mwaka mmoja baada
ya Dk Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa akishikilia wadhifa huo
Lusekelo Mwaseba.
“Uteuzi wa Mwenyekiti mwingine wa Bodi ya Wakurugenzi wa TRA na Bodi ya Mamlaka hiyo utatangazwa baadaye,” ilieleza taarifa ya Ikulu iliyotolewa Jumapili asubuhi sana.
Akihutubia
jana katika Mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT)
kwenye Makao Makuu ya chuo hicho, Bungo wilayani Kibaha katika mkoa wa
Pwani, Dk Magufuli alisema aliitumbua bodi hiyo kutokana na kukiuka
taratibu.
Alieleza
kuwa kitendo chao cha kuidhinisha fedha hizo kuwekwa kwenye benki
tofauti, ni tofauti na maelekezo kwani huo ndio ulikuwa mchezo
unaofanywa na taasisi na mashirika mbalimbali.
“Sasa
sifahamu kama Chuo Kikuu Huria na nyinyi mmekuwa mkiweka fedha za
maendeleo katika Fixed Deposit Account, (akaunti maalumu) lakini huo
ndio umekuwa ni mchezo, juzi hapa tumekuta fedha kiasi cha Shilingi
bilioni 26 zilizokuwa zimetolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa
ajili ya matumizi ya TRA, zikapelekwa kwenye benki tatu kama Fixed
Deposit Account na Bodi ya TRA ikapitisha, ndio maana nilipozipata hizo
taarifa, fedha nikachukua na Bodi kwa heri.
“Hata
kwa sasa hivi Waziri (wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako) upo hapa,
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ambayo ilianzishwa kwa sababu maalumu,
inachangiwa fedha wakati kuna fedha zao wameziweka kwenye Fixed Deposit
Account, Waziri hiyo ni message sent and Delivered,” alisisitiza Rais Magufuli.
Alisema
kumekuwa na mchezo wa wakuu wa taasisi mbalimbali kuchukua fedha na
kuziwekwa kwenye akaunti maalumu ambako serikali inakwenda kukopa kwa
gharama kubwa.
“Kwa
sasa huu ndio mchezo ambao unachezwa na kuisababishia serikali kukosa
fedha jambo ambalo serikali haiko tayari kuona matumizi mabaya ya fedha
zake,” alieleza Dk Magufuli ambaye anafahamika kwa kusisitiza kubana
matumizi ya serikali na kukerwa na ukiukwaji wa taratibu za uendeshaji
wa serikali.
Alisema
mchezo huu umekuwa ukiipa serikali gharama kubwa kwa sababu ya kukopa
fedha kwenye benki kwa gharama kubwa na kupotosha upatikanaji wa mapato.
“Naomba
mtuombee tuendelee kutumbua kwani nchi ilifika mahali pabaya ambapo
wanaweza kuitisha vikao hata Ulaya na kutokana na tumbua hii mapato
yameongezeka kutoka trilioni 1.2 na kufikia 1.8 ambapo uchumi
umeimarika,” alieleza Dk Magufuli.
Alisema
uchumi umeimarika na unatakiwa ukue kwa asilimia 7.2, lakini hadi robo
ya mwaka huu umekua kwa asilimia 7.9 na kuwa moja ya nchi ambazo uchumi
wake unakua kwa kasi, ambazo kati ya nchi tano imekuwa ya pili baada ya
Ivory Coast.
Aidha,
alisema thamani ya fedha imepanda na kwamba wanaopotosha juu ya fedha
ni wale waliokuwa wanapiga dili ambao kwa sasa hawana nafasi. Jumla ya
wahitimu 4,027 walihitimu na kutunukiwa shahada mbalimbali na Mkuu wa
Chuo Kikuu Huria Tanzania, Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda.
No comments:
Post a Comment