Mahakama ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imewaachia huru viongozi na wanachama 17 wa Chadema walikokuwa wakikabiliwa na mashitaka ya kujaribu kushawishi kutenda kosa Agosti 25 katika ofisi ya wilaya ya chama hicho Mnadani mjini hapa.
Wanachama
waliachwa jana na Hakimu Tumaini Marwa aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo
baada ya upande wa mashitaka chini ya Mwendesha Mashitaka wa Polisi,
Nassib Swedy kushindwa kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo huku wakitoa
sababu mbalimbali.
Swedy
alidai kuwa washitakiwa hao wakiwa kwenye ofisi yao siku hiyo saa 7
mchana walipanga kufanya maandamano na mikutano ya Ukuta, ambayo
ingehatarisha amani na utulivu wilayani humo na Taifa kwa ujumla.
Hata
hivyo, washitakiwa hao ambao awali walifikishwa mahakamani hapo Agosti
26 chini ya ulinzi mkali wa Polisi, walikana mashitaka na kunyimwa
dhamana, walidhaminiwa Septemba 2 baada ya kukamilisha masharti ya
dhamana ya kuwa na mdhamini mmoja wa kuaminika ambaye alisaini bondi ya
Sh milioni tano.
Akitoa
uamuzi huo jana, Hakimu Marwa alitupilia mbali maombi ya upande wa
mashitaka yaliyokuwa yakiomba ahirisho la kesi hiyo kwa mara nyingine
ukidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Alisema
amri ya mwisho aliyoitoa ilikuwa ahirisho la Novemba 4 hivyo upande wa
mashitaka umeshindwa kutekeleza amri ya Mahakama na kwa maana hiyo,
anawaacha huru washitakiwa wote chini ya kifungu cha sheria ya Mwenendo
wa Makosa ya Jinai kifungu cha 225 (5) sura ya 20.
“Kifungu
hiki kilichowaacha huru washitakiwa hakizuii Polisi kuwafikisha
mahakamani tena washitakiwa kwa kosa hilo, iwapo watakuwa wamekamilisha
uchunguzi juu ya shauri linalowakabili,” alisema Hakimu Marwa.
Hata
hivyo, wakati uamuzi unatolewa wakili wa washitakiwa hao, Martine
Sabini aliyekuwa akiwakilisha washitakiwa wote hakuwapo mahakamani,
lakini alikuwa ameshawasilisha ombi mbele ya Mahakama hiyo kuomba
waachiwe huru kwa sababu ya upande wa mashitaka kushindwa kukamilisha
upepelezi kwa muda mwafaka.
Walioachiwa
huru ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema wa Wilaya ya Maswa, Peter
Shiyo (39), Katibu wa Chadema wa Wilaya, Flora Msuka (31), Katibu wa
Bawacha wa Wilaya, Elias Matondo (37) na Katibu Mwenezi wa Maswa
Mashariki, Waziri Peter (46).
Wengine
ni Bundala Baya (30), Edward Makoye (63), Sylvester Ngwege (60), Frank
Makaranga (31), Selemani Kombe (39) na Mapambano Jackson (37).
Pia Nkuba Magwila (40), Ndebile Paul (27), Edgar Ngasa (32), Lucas Nkuba (39), Laurent Mahembo (36) na Mwajuma Said (40).
Baada
ya kuachwa, Shiyo aliishukuru Mahakama kwa kutenda haki akilitaka Jeshi
la Polisi kuacha kunyanyasa viongozi wa vyama vya upinzani kwa kufanya
kazi kwa hisia na matokeo yake, wanaitia aibu Serikali kwa kushindwa
kesi mahakamani.
No comments:
Post a Comment