JESHI
la Polisi Mkoa wa Arusha linamshikilia mkazi wa Olasiti, jijini Arusha,
Hamisi Amani (17), kwa tuhuma za kumuua mwenzake wakati wakigombea
soda.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha,
Charles Mkumbo, tukio hilo lilitokea Desemba 25, mwaka huu, saa mbili
usiku katika eneo la Kwa Morombo.
Kamanda
Mkumbo alimtaja marehemu kuwa ni Novatus Tadei (26), mkazi wa Kwa
Morombo na kwamba aliuawa kwa kuchomwa kisu kifuani upande wa kushoto.
“Marehemu na mtuhumiwa walikuwa wapishi kwenye kampuni inayojulikana kwa jina la ZZ Catering inayomilikiwa na Bashiri Ally.
“Siku
ya tukio, marehemu pamoja na wafanyakazi wengine, akiwamo mtuhumiwa,
baada ya kumaliza kazi waliyokuwa wanafanya, walipanda gari lenye namba
za usajili T 375 CHH, aina ya Toyota Hiace wakirejea nyumbani.
“Wakiwa
ndani ya gari hilo, mtuhumiwa Hamis aligundua kuwa soda aliyokuwa
ameiweka ndani ya begi lake, haipo na kuanza kuhisi marehemu ndiye
aliyeichukua.
“Kwa
hiyo, ulizuka ugomvi baina yao na kuanza kutukanana matusi. Wakati
ugomvi huo ukiendelea, mtuhumiwa alimkaba marehemu na kuchukua kisu
wanachotumia kwenye shughuli zao za mapishi kilichokuwa ndani ya vyombo
na kumchoma kifuani.
“Baada
ya kuchomwa kisu, Tadei alianguka chini na jitihada za wafanyakazi
wenzake waliokuwamo ndani ya gari hilo kuokoa maisha yake
zilishindikana, kwani alifariki wakati anapelekwa hospitali kwa ajili ya
matibabu,” alisema Kamanda Mkumbo.
Alisema
mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya
Mount Meru na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya
uchunguzi kukamilika.
No comments:
Post a Comment