Jana
December 27 2016 mbunge wa kigoma mjini na kiongozi mkuu wa chama cha
ACT Wazalendo Zitto Kabwe na mke wake wamepata mtoto wa kike ambaye
wamempa jina la Josina – Umm Kulthum.
Zitto Kabwe kupitia ukurasa wake wa facebook amesimulia alichokutana nacho hospitalini saa chache kabla ya mke wake kujifungua, haya ni maneno yake….
"Usiku
wa kuamkia tarehe 26 Desemba 2016 mke wangu alipata uchungu wa uzazi.
Nikampeleka hospitali moja hapa Masaki. Hakuweza kujifungua siku hiyo
bali tulikaa hospitali mpaka tarehe 27 Desemba, saa moja dk 45 asubuhi
alipojifungua mtoto wetu wa kike Josina- Umm Kulthum.
"Masaa
ya jioni tarehe 26/12/2016 nikiwa napiga soga na Naibu Katibu Mkuu wa
ACT Wazalendo Msafiri Mtemelwa na shemeji yangu mmoja mbele ya
hospitali, wakaja watu 3. Watu hao mmoja mwanaume na wengine wanawake
walikuwa na mtoto mdogo.
"Mwanaume
huyu alikuwa amembeba mtoto akiwa na taharuki kubwa na mama mmoja mtu
mzima na mwingine wa umri wa miaka 30 hivi walikuwa wakilia. Wakaingia
hospitalini kwa kasi. Tukaambiana pale kuwa huyu binti atakuwa mahututi.
Tukaendelea na soga.
"Mara
kina mama wale wakatoka, wanapiga mayowe “mtoto hana damu” na ilitakiwa
damu ya haraka Group A+. Wenzangu hawakuwa group hilo au group
linaloweza kupeana damu. Mimi sikuwa najua/kukumbuka Group langu.
"Nikawaambia
kina mama wale kuwa ngoja nijaribu kupima group langu na pia kuona kama
damu yangu inaweza kuokoa maisha ya mtoto yule malaika za mungu.
Nikaingia maabara nikapima. Baada ya dakika 10 Hivi nikaitwa kuambiwa
damu yangu ni group sawa na mtoto yule na kwamba ni safi inafaa wanitoe
muda ule ule ili kumuwahi mtoto. Nikatoa nusu lita muda ule ule.
"Baadaye
nikaenda kumjulia Hali mtoto yule, nikaambiwa anaitwa Rahma. Ana umri
wa miaka 2 na miezi 3. Nikawatakia kheri wazazi wake ( kumbe yule
mwanaume ndie baba wa mtoto na msichana mama yake. Yule bi mkubwa
nadhani ni bibi ya Rahma, sina hakika).
"Leo
(Jana) asubuhi baada ya mke wangu kujifungua, nikaenda kumwona Rahma
wodini. Nimemkuta anaendelea vizuri, anakula na kuongea. Mola ampe umri
mrefu zaidi yeye na wazazi wake. Amwondolee maradhi na akue katika
maadili mema ya dini.
"Namshukuru
mola kuniweka mahala sahihi na wakati sahihi hivyo kuweza kufanya ibada
hii ya kumsaidia binti Rahma. Lau kama sikuwa nimechagua jina la binti
yangu mapema, ningemwita Rahma. Hata hivyo inshallah Rahma atakuwa dada
yake Umm Kulthum-Josina.
"Naishauri
Serikali itengeneze kanuni za kuhakikisha kila hospitali inakuwa na
akiba ya damu ya kutosha na mgonjwa mwenye kuhitaji apewe kwanza damu
kabla ya kutafuta watu wa kuchangia kiwango husika.
"Juhudi
za kuchangia damu kwa hiari ziongezeke kama tufanyavyo wanachama wa ACT
Wazalendo ambao kila mwaka Wiki ya kwanza ya Mwezi Mei hujitolea damu
kwa hiari kwenye hospitali za umma nchini kote.
"Aidha
nimepata somo kubwa kwamba ni muhimu Sana kujua Group lako la damu na
kuwa na kumbukumbu nalo kwani inaokoa muda pindi damu ikitakiwa kwa
haraka. Sasa najua Group langu, ilikuwa ni makosa makubwa na uzembe wa
hali ya juu kwangu kutojua ‘ blood group ‘ yangu. Nawasihi Watanzania
wenzangu na mie msiojua blood group, mjue sasa kwani hatujui Siku wala
Saa."
No comments:
Post a Comment