Wakati
Jeshi la Polisi likiendelea kutoa tahadhari ya mara kwa mara kwa
madereva kuwataka waongeze umakini hasa katika kipindi hiki cha kuelekea
msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.
Ajali mbaya ya mabasi la abiria ilitokea jana na kusababisha vifo vya watu saba huku wengine 12 wakijeruhiwa vibaya.
Kwa
mujibu wa mashuhuda, saba waliofariki dunia ni wanaume watano akiwamo
dereva wa Toyota Hiace aliyetajwa kwa jina la Hassan na wengine wakiwa
ni mtoto mdogo na mwanamke anayedhaniwa kuwa ni wa mtoto aliyefariki
dunia.
Tukio
hilo lililotokea jana majira ya saa 11:00 alfajiri, ikiwa ni siku nne
tu kabla ya siku ya sikukuu ya Krismasi, lilitokea katika Kijiji Cha
Kabeba, Kata ya Mwakizega, Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma
baada ya basi kubwa la abiria aina ya Scania la kampuni ya Saratonga
(namba T384 BMG) kugongana uso kwa uso na basi dogo aina ya Toyota Hiace
‘kipanya’, lenye namba za usajili T237BCE.
Taarifa
zilizothibitishwa na Polisi kupitia kwa Kaimu Kamanda wake mkoani humo,
Sweatbert Njewike, abiria wote waliofariki dunia walikuwa katika basi
dogo lililokuwa likisafiri kutoka Kigoma Mjini kwenda katika Kijiji cha
Lilagala, Wilaya ya Uvinza mkoani humo.
Majeruhi
walipelekwa kwenye Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Kigoma wakiwa ni wa
kutoka mabasi yote mawili. Basi kubwa lilikuwa likitokea eneo la kijiji
cha Lilagala kwenda Kigoma Mjini.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda Njewike, uchunguzi kuhusiana na ajali hiyo bado unaendelea kabla hatua zaidi hazijachukuliwa.
Hata
hivyo, kamanda huyo aliongeza kuwa taarifa za awali zinaonyesha kuwa
chanzo ni uzembe na ubabe wa madereva wa magari hayo baada ya wote
wawili kukataa kupeana nafasi ya kupita kwa zamu kwenye daraja jembamba
katika eneo hilo na mwishowe kugongana uso kwa uso wakati kila mmoja
akijaribu kupita kwa kasi.
Kutokana
na ajali hiyo, Kamanda huyo aliwataka madereva mkoani humo kuzingatia
sheria za barabarani ili kujiweka mbali na ajali zinazoepukika na pia
kutumia busara kwa kupeana nafasi wakati wanapokatiza kwenye maeneo tata
kama ya kwenye madaraja madogo na kona kali.
Mganga
Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Kigoma, Maweni Kibaya,
alisema jana kuwa waliwapokea watu waliojeruhiwa katika ajali hiyo na
kwamba walikuwa wakiendelea kuwatibia huku baadhi yao wakiwa na majeraha
makubwa katika sehemu mbalimbali za miili yao.
No comments:
Post a Comment