
Na Okuly Julius, OKULY BLOG - Dodoma
Tume ya Utumishi wa Umma inatarajia kuanza kusikiliza rufaa na malalamiko ya watumishi wa umma katika mkutano wake wa tatu wa mwaka wa fedha 2025/2026 utakaofanyika jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari Machi 18,2026 jijini Dodoma , Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, John Mbisso, amesema mkutano huo unatarajiwa kuanza Machi 23, 2026 na kuhitimishwa Aprili 15, 2026 katika ukumbi wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) uliopo eneo la Ndejengwa.

Amesema lengo la mkutano huo ni kusikiliza na kutoa maamuzi ya rufaa pamoja na malalamiko yaliyowasilishwa na watumishi wa umma ambao hawakuridhika na maamuzi ya waajiri wao, mamlaka za ajira pamoja na mamlaka za nidhamu.
Amefafanua kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298 (Marejeo ya mwaka 2023), Tume ina jukumu la kupokea, kusikiliza na kuamua rufaa na malalamiko kwa lengo la kuhakikisha haki inatendeka kwa watumishi wa umma.
Aidha, Mbisso amewahimiza warufani na warufaniwa kufika mbele ya Tume kutoa ufafanuzi wa ziada kuhusu hoja zao ili kuwezesha maamuzi ya haki na yenye kuzingatia ushahidi.

No comments:
Post a Comment