Na,Okuly Julius ,Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka amewataka wadau wa elimu mkoani hapa wakiwemo maafisa elimu na waratibu elimu kuwa na ubunifu ili kuongeza kiwango cha ufaulu .
Mtaka amebainisha hayo leo Februari 18,2022 jijini Dodoma wakati akizungumza katika kikao kazi na waratibu na maafisa elimu mkoani Dodoma.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema ili kiwango cha elimu kiendelee kuimarika mkoani Dodoma hakuna budi kwa kila mmoja kuwa na ubunifu wake huku akiwataka maafisa elimu hao kuwaruhusu walimu pindi wanapotaka kujiendeleza.
“Suala la elimu lazima utumie ubunifu na mbinu nyingi,hauwezi kukariri tu St.Francis wanakaririshwa lazima patengenezwe mazingira ya ufaulu kulingana na mazingira uliyo nayo,unakuta unamzuia mwalimu kwenda kujiendeleza wakati ana hela zake umzuie kwa nini badala ya kufurahi huyo mwalimu anaenda kuongeza ujuzi”amesema.
Aidha ,Mtaka ametolea mfano wakati akiwa mkoani Simiyu kulikuwa na mtoto alikuwa anapata daraja sifuri lakini alitengenezewa ubunifu kwa kumpa moyo pamoja na mitihani ya ujirani mwema hali iliyosaidia kiwango cha ufaulu na kupata daraja la pili.
Awali afisa elimu mkoa wa Dodoma Gift Kyando amesema wao kama wasimamizi wa elimu wapo tayari kupokea maagizo na maelekezo ya Mkuu wa mkoa katika kuhakikisha kiwango cha ufaulu kinaongezeka mkoani Dodoma.
No comments:
Post a Comment