KWENYE ZIARA YA NAIBU KATIBU MKUU WA WIZARA YA MADINI, KURUGENZI ZA TUME YA MADINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, March 4, 2022

KWENYE ZIARA YA NAIBU KATIBU MKUU WA WIZARA YA MADINI, KURUGENZI ZA TUME YA MADINI




_Awataka watumishi Tume ya Madini kulinda rasilimali za madini kwa nguvu zote_ 

 _Ataka kasi ya ubunifu kuongezeka kwenye usimamizi Sekta ya Madini_ 

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amewataka watumishi wa Tume ya Madini nchini kulinda rasilimali za madini kwa kusimamia kwa ubunifu huku wakitanguliza maslahi ya wananchi mbele ili mchango wa Sekta ya Madini uzidi kukua kwenye Pato la Taifa.

Mbibo ametoa rai hiyo leo kwenye ziara yake katika Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira na Kurugenzi ya Ukaguzi na Biashara ya Madini zilizopo chini ya Tume ya Madini jijini Dodoma yenye lengo la kujifunza kwa mapana zaidi namna Tume ya Madini inavyoendesha shughuli zake na kutatua changamoto mbalimbali.

Alisema kuwa lengo la Wizara ya Madini ni kuona wananchi hasa walio masikini wananufaika na wingi wa rasilimali nyingi za madini zilizopo kupitia uboreshaji wa huduma za jamii kama vile maji, umeme, afya, barabara na shule na kusisitiza kuwa ni vyema wakafanya kazi kwa uadilifu huku wakiwafikiria wananchi waliopo vijijini.

"Ni lazima mfahamu ya kuwa wananchi wengi hasa walio vijijini wana mategemeo makubwa sana kwenye Wizara ya Madini hasa kwenye eneo la usimamizi wa rasilimali za madini, ninyi kama wataalam ni muhimu mkatanguliza maslahi ya umma wa watanzania badala ya binafsi ili manufaa ya rasilimali za madini yaonekane" alisema Mbibo.

Katika hatua nyingine aliwataka watumishi wa Tume ya Madini kuwa waadilifu kwenye utendaji kazi huku wakifuata sheria na kanuni za madini.

Aidha, aliwataka watumishi wa Tume kujiendeleza kielimu na kujifunza teknolojia mpya ili kuongeza kasi inayoendana na ulimwengu wa sasa na kuvutia zaidi wawekezaji wengi kuja kuwekeza kwenye Sekta ya Madini.

Aliendelea kusema kuwa Wizara ya Madini itaendelea kutatua changamoto mbalimbali za Taasisi zake kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini.

Awali akizungumza kwenye ziara hiyo Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini, Venance Kasiki sambamba na kumpongeza Naibu Katibu Mkuu kwa kutembelea Kurugenzi za Tume na kusikiliza changamoto alisema kuwa Kurugenzi imejikita kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini hasa kwenye biashara ya madini na kuhakikisha watanzania wananufaika kupitia Ushirikishwaji wa Watanzania kwenye Sekta ya Madini (Local Content)

"Mimi na timu yangu ya wataalam sambamba na kusimamia biashara ya madini na kodi mbalimbali tumeweka nguvu kubwa kwenye kuhakikisha watanzania wanashiriki kwenye uwekezaji katika Sekta ya Madini kupitia utoaji wa huduma mbalimbali kwenye migodi ya madini kama vile vyakula, ulinzi, usafiri n.k" alisema Kasiki

Aliongeza kuwa katika kuongeza kasi ya utendaji kazi, Kurugenzi ya Ukaguzi na Biashara ya Madini imebuni mfumo mpya utakaotumika katika kuwasilisha mipango ya ushirikishwaji wa watanzania kwenye Sekta ya Madini (Local Content)

Katika ziara yake Naibu Katibu Mkuu Mbibo aliambatana na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu kutoka Wizara ya Madini, Issa Nchasi na Mkurugenzi wa Huduma za Tume ya Madini, William Mtinya.




No comments:

Post a Comment