Na Okuly Julius Dodoma
Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu Kamisaa wa Sensa Tanzania bara Anna Makinda amewataka watendaji wa Mitaa,Kata na Tarafa kuhakikisha wanawapitisha wasimamizi na makarani wenye sifa na kuacha tabia ya kuwaweka ndugu zao ambao hawana sifa.
Ameyasema Hayo wakati akizungumza na Watendaji wa kata,mitaa,tarafa pamoja na madiwani wote wa halmashauri ya jiji la Dodoma katika kikao kilichofanyika hii leo March 22,2022 jijini Dodoma.
Amesema katika kuzingatia suala la usawa Waziri Mkuu atawaandikia barua wakuu wa mikoa itakayotoa maelekezo kuhusu utekelezaji wa zoezi la sensa ya watu na makazi ili kuweka uzito katika jambo hili muhimu kwa taifa.
"Sisi hapa ni mashahidi mtaani kwetu Kuna watu wengi waliohitimu masomo na hawana kazi mtaani na Wana vigezo vyote vinavyostahili,hivyo mwenye vigezo achukuliwe akasaidie kazi hii na kujipatia kipato na si kuchukua ndugu na jamaa zetu ikiwemo watoto wa wenyeviti,madiwani na watendaji".amesema Makinda
Mama Makinda ameongeza kuwa sensa ya watu na makazi ni muhimu Kwa Taifa kwasababu itasaidia kuwa na takwimu sahihi Kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla hivyo ni muhimu watu wote wakahesabiwa.
"Usipohesabiwa utakuwa unakula chakula cha wenzako kila siku hivyo utawakosesha wenzako huduma kwa kuwa hautakuwa kwenye mahesabu hivyo serikali inapoleta huduma sehemu wewe unakuwa haupo utakuwa unakula vya wenzako tu;" ameongeza Makinda
Pia ameweka wazi utaratibu wa namna ya kuajiri Makarani wa Sensa mwaka huu kuwa ni kwa njia ya Kompyuta hivyo hakuna namna yeyote ya kumpenyeza mtu na zoezi hilo litakuwa la wazi na haki kwa sababu kila kitu kitafanyika mtandaoni.
Kwa upande Kaimu Mkurugenzi wa sensa ya watu na takwimu za jamii Ruth Minja Kwa niaba ya mtakwimu mkuu wa Serikali Dkt Libena Chua amesema kuwa maandalizi ya sensa ya watu na makazi yanaendelea vizuri ikiwemo utengaji wa maeneo ya kuhesabia watu.
"Maandalizi ya sensa hii yanaendelea vizuri,katika utekelezaji wa sensa ya watu na makazi Kuna awamu kuu tatu awamu ya kwanza ni Ile ya kabla ya kuhesabu watu,awamu ya pili ni Ile ya kuhesabu watu na ya tatu ni Ile baada ya kuhesabu watu sisi tuko katika hii awamu ya kwanza ikijumuisha utengaji wa maeneo madogo madogo ya kuhesabia watu hivyo tuko vizuri"amesema Minja
Aidha amesema Kwa Mara ya kwanza Serikali ya Tanzania inafanya sensa yake kidijitali ikiwemo mfumo wa kidijitali wa ukusanyaji wa taarifa Kwa kuweka kwenye vishikwambi na sio makaratasi kama ilivyozoeleka katika sensa zilizopita.
No comments:
Post a Comment