MWAKA MMOJA WA MAFANIKIO KWA SERIKALI YA AWAMU YA SITA KATIKA ENEO LA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA, MHE.JENISTA MHAGAMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, March 16, 2022

MWAKA MMOJA WA MAFANIKIO KWA SERIKALI YA AWAMU YA SITA KATIKA ENEO LA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA, MHE.JENISTA MHAGAMA


Waziri wa nchi,Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh.Jenista Mhagama( MB) wakati akitoa taarifa kuhusu Mafanikio ya mwaka mmoja wa serikali ya awamu ya sita yaliyopatikana kwenye eneo la Utumishi wa Umma na Utawala Bora Wizara hiyo kwa waandishi wa habari jijini Dodoma hii leo March 16,2022.


Waziri wa nchi,Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh.Jenista Mhagama( MB) akizungumza na Waandishi wa habari katika ofisi za Utumishi Mtumba jijini Dodoma


Baadhi ya Waandishi wakisikiliza taarifa ya Waziri wa nchi,Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh.Jenista Mhagama( MB

Na Okuly Julius, Dodoma

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha mwaka mmoja imepata mafanikio makubwa katika eneo la Utumishi wa Umma na Utawala Bora,mafanikio haya yanatokana na azma ya Mhe. Rais ya kutaka kuujenga utumishi wa umma wenye tija katika maendeleo ya taifa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa nchi,Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh.Jenista Mhagama( MB) wakati akitoa taarifa kuhusu Mafanikio ya mwaka mmoja wa serikali ya awamu ya sita yaliyopatikana kwenye eneo la Utumishi wa Umma na Utawala Bora Wizara hiyo kwa waandishi wa habari jijini Dodoma hii leo March 16,2022.

Mhe.Mhagama amepongeza Mhe. Rais na kuongeza kuwa amedhihirisha kuwa yeye ni kiongozi bora, muadilifu, mbobezi, mzalendo, mchapakazi, mcha Mungu, mwenye nia na maono makubwa ya kuleta ustawi wa taifa na maendeleo ya Watanzania,Tunamuombea Baraka kwa Mwenyezi Mungu ampe afya njema na maisha marefu.

Pia amesema kuwa ,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma ina jukumu la kisera la kusimamia uendelezaji sera katika Utumishi wa Umma, Utawala wa Utumishi wa Umma, Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Mishahara, Usimamizi wa Mifumo ya Uendeshaji wa Serikali, Usimamizi wa Mifumo ya Utendaji Kazi wa kila Siku Serikalini, Uendelezaji Rasilimaliwatu, Ukuzaji wa Maadili katika Utumishi wa Umma, Usimamizi wa Serikali Mtandao na Usimamizi wa Anuai za Jamii katika Utumishi wa Umma.

Ameongeza kuwa,Ofis ya Rais pia ina dhamana ya kusimamia masuala ya Utawala Bora na Vilevile ina jukumu la kusimamia taasisi fungamanishi zinazoshiriki katika kuleta maendeleo na ustawi wa wananchi .

Serikali ya Awamu ya Sita, pamoja na kuzingatia dhamira aliyoionyesha Mhe. Rais wakati akihutubia Bunge la 12 kwa mara ya kwanza zimedhihirisha kasi ya kiwango cha juu cha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025, Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano (2021-2026) pamoja na maelekezo ambayo Mhe. Rais amekuwa akiyatoa katika Ofisi hiyo.

Ambapo mpaka sasa kupitia ,Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imefanikiwa pakubwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Kusimamia mageuzi katika Utumishi wa umma katika kutazama maslahi ya watumishi, ikiwemo suala la upandishaji vyeo na mishahara, kuangalia upya Mfumo wa Wazi wa Upimaji wa Utendaji Kazi wa Watumishi (OPRAS) ili kupata mfumo sahihi wa usimamizi wa utendaji kazi wa Watumishi wa Umma nchini pamoja nakuimarisha mifumo ya uwajibikaji, ambayo itahakikisha Viongozi na Watumishi wa Umma katika ngazi zote wanawajibika kwa hiari katika kufikia malengo waliyojiwekea katika taasisi zao.

Pia Wamefanikiwa kuimarisha utekelezaji wa Sera ya Serikali Mtandao na kujenga mifumo ya TEHAMA inayohusu uendeshaji wa Serikali wa kila siku, kurahisisha utoaji wa huduma bora kwa umma na kuimarisha maadili ya utendaji kazi katika utumishi wa umma kwa kutumia mifumo, kuhuisha sera na kanuni za Utumishi wa Umma ili ziendane na mazingira na mahitaji ya sasa ya ujenzi wa uchumi na maendeleo ya taifa,Kujenga uwezo wa Viongozi na Watumishi wa Umma ili waweze kuwatumikia wananchi kikamilifu,Kubuni mbinu na mikakati ya kuhakikisha Watumishi wa Umma wanapata makazi bora kwa gharama nafuu.

Pamoja na hayo pia wamefanikiwa Kuendelea kusimamia upatikanaji wa rasilimaliwatu yenye sifa stahiki katika Utumishi wa Umma,Kuendelea kuhakikisha haki inatendeka kwa Watumishi wa Umma wenye malalamiko dhidi ya waajiri wao,Kuendelea kujenga mifumo imara ya utunzaji wa kumbukumbu, nyaraka na amali za taifa pamoja na kuimarisha mifumo ya utunzaji wa siri za Serikali kwa Viongozi na Watumishi wa Umma,Kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa katika Utumishi wa Umma na taifa kwa ujumla,Kuendeleza juhudi za kupambana na umaskini na kuimarisha uchumi wa kaya maskini kupitia miradi ya TASAF.

"Katika eneo la Kusimamia mageuzi katika Utumishi wa Umma na kutazama maslahi ya watumishi, ikiwemo suala la upandishaji vyeo na mishahara, Mhe. Rais kupitia Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mhe. Rais alituelekeza kuwapandisha vyeo/madaraja Watumishi 190,781 wenye sifa stahiki. Mhe. Rais aiamua tutumie jumla ya shilingi bilioni 39,649,988, 204 na kazi inaendelea" Amesema Mhe.Mhagama

"Kulipa madeni ya mishahara ya Watumishi wa Umma 65,394 yenye thamani ya shilingi bilioni 91,087,826,006.34,Kuwabadilisha kada Watumishi wa Umma 19,386 na kuwalipa mishahara mipya yenye thamani ya shilingi bilioni 1,330,306,572,Kutoa vibali12,336 vya ajira mpya na mbadala ambapo jumla ya shilingi bilioni 7,761,869,809 zimelipwa,Kuwapunguzia kodi watumishi wa umma kutoka asilimia 9 mpaka 8"Ameongeza

Aidha, katika kipindi hiki Serikali imeanza ujenzi wa Mfumo mpya wa Usimamizi wa Utendaji kazi katika ngazi ya Taasisi Public Institutions Performance Management Information System (PIPMIS). Mfumo huu ni makubaliano ya kimaandishi kati ya Serikali na Taasisi ya Umma kuhusu malengo ambayo Taasisi husika itayatekeleza katika kipindi cha mwaka mmoja. Makubaliano hayo yatakuwa kati ya viongozi wakuu wa Taasisi na Viongozi wao wanaowasimamia katika masuala ya kisera na utendaji wa kila siku.

Utekelezaji wa Mfumo wa Huu wa PIPMIS utaongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa sera, mikakati na vipaumbele vya taasisi, sekta na taifa kwa ujumla; kuimarisha utamaduni unaojali matokeo; na kuleta matumizi bora ya rasilimali za umma,Manufaa haya yatatokana na kuwepo kwa vigezo na viashiria vya kupima utendaji wa taasisi katika maeneo hayo, kulinganisha na kushindanisha utendaji wa taasisi na kutoa Tuzo za utendaji mzuri kila mwaka.

Mhe.Jenista Mhagama ameongeza kuwa ili kupata mfumo sahihi wa kupima utendaji kazi wa Watumishi wa Umma na taasisi kama ilivyoelekezwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma imeunda timu ya Wataalam wabobezi ambao wameanza kutengeneza mifumo mipya ya kielektroniki ya usimamizi wa utendaji kazi wa Watumishi wa Umma na taasisi za umma.

Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma imefanikiwa kujenga Mfumo wa Sema na Waziri wa UTUMISHI kwa lengo la kuwawezesha watumishi na wananchi kuwasiliana moja kwa moja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuhusu masuala mbalimbali ya Utumishi na Utawala.

Aidha mfumo huu unampa fursa Waziri wa Utumishi na Utawala Bora kufuatilia namna masuala ya utumishi na Utawala Bora yaliyowasilishwa na wananchi na watumishi wa Umma yalivyofanyiwa kazi na kumuwezesha Waziri kufuatilia hali ya uadilifu na uwajibikaji wa watumishi wa umma katika kushughulikia masuala mbalimbali ya utumishi na utawala bora. Mfumo huu pia unamuwezesha Waziri wa Utumishi na Utawala Bora kuongea moja kwa moja na mlalamikaji ili kujua ni kwa namna gani tatizo lake limefanyiwa kazi na kuchukua hatua stahiki.

Pia imeanzisha mifumo mingine kama vile mfumo wa e-mrejesho,Mfumo wa Dawati la huduma kwa mteja maarufu kama UTUMISHI Call Center ,Mfumo wa Huduma mtandao kwa watumishi (Watumishi Portal) pamoja na mifumo mingingine mingi yenye lengo la kuboresha uwajibikaji wa hiari na wa haki kwa Watumishi wa Umma.
Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (WHMTH) imeanzisha mpango wa kuwa na vituo mahsusi vya kutolea huduma kwa wananchi vinavyojulikana kama Vituo vya Huduma Pamoja. Hadi mwezi Machi, 2022 vituo viwili (2) vya Huduma Pamoja vimeanzishwa katika majengo ya Posta Jijini - Dar es Salaam na Posta Jijini - Dodoma.

Huduma zilizoanza kutolewa katika Vituo hivyo ni pamoja na Huduma za RITA, Huduma za NIDA, Leseni za Biashara zinazotolewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Huduma za Uhamiaji, Huduma za NSSF, Huduma za NHIF na Huduma za BRELA. Vituo hivi vya kutolea huduma sehemu moja vitaongeza ufanisi, ubora na urahisi wa kupata huduma zinazotolewa na Serikali.

Sambamba na uanzishwaji wa Vituo vya Huduma Pamoja, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa kushirikiana na WHMTH imeanza kuandaa mkakati kujumuisha makundi yenye mahitaji maalumu katika huduma za kidigitali zinakazotolewa na Serikali. Hadi kufikia mwezi Machi, 2022, kazi ya kukusanya mahitaji ya makundi hayo imeanza katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Taarifa zinazokusanya zinalenga kubainisha mahitaji ya makundi maalum ili kuyajumuisha katika mradi wa Tanzania ya Kidigitali.

Hata hivyo Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma kupitia Tume ya Utumishi wa Umma imeendelea kuhakikisha haki inatendeka kwa Watumishi wa Umma wenye malalamiko dhidi ya waajiri wao ambapo Katika kipindi hiki imeshughulikia na kutolea uamuzi rufaa 313 na malalamiko 174 ya watumishi waliochukuliwa hatua na mamlaka zao za nidhamu.
Pia Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma kupitia Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa imeendelea na jukumu la kujenga mifumo imara ya utunzaji wa kumbukumbu, nyaraka na amali za taifa pamoja na kuimarisha mifumo ya utunzaji wa siri za Serikali kwa Viongozi na Watumishi wa Umma.

Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja Idara hiyo imepata mafanikio ya Kuweka na kuhuisha Mfumo wa Utunzaji wa Kumbukumbu za Kiutendaji (Keyword Filing System) katika Taasisi za Umma hamsini na saba (57); na Mfumo wa Masijala Mtandao (e-File Management System) katika Taasisi za Umma ishirini (20).

Katika kutekeleza maagizo ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu utunzaji wa siri za Serikali, Ofisi ya Rais, menejimenti ya Utumishi wa Umma imetoa Waraka wa Utumishi wa Umma Na. 2 wa Mwaka 2021 kuhusu Mifumo Rasmi ya Mawasiliano Serikalini.

Aidha, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa imefanya tathmini na ufuatiliaji wa mifumo ya utunzaji wa kumbukumbu katika Taasisi za Umma 152 kwa lengo la kujua hali halisi ya utunzaji kumbukumbu katika taasisi hizo. Vilevile, Idara imetoa elimu kwa taasisi za umma ili kuzikumbusha wajibu wao wa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya utumiaji na utunzaji wa kumbukumbu.

Kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Kumbukumbu cha Kanda ya Ziwa Mwanza ambacho kina uwezo wa kuhifadhi jumla ya majalada 117,600 yaliyoko kwenye mfumo wa karatasi. Aidha, Kituo hicho kimewekewa miundombinu wezeshi ya kuhifadhi nyaraka kidigitali na ununuzi wa vifaa vya kuhifadhi nyaraka katika mifumo hiyo ya kidigitali unaendelea.

Pamoja na hayo Idara imeweza Kutambua, kukusanya, kutunza na kuhifadhi kumbukumbuku na vitu vya Waasisi wa Taifa kutoka katika Taasisi za Umma na watu binafsi ili kuwaenzi Waasisi wa Taifa letu,Vilevile Idara imekusanya jumla ya kumbukumbu 821 za Waasisi wa Taifa (Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume) kwa ajili ya matumizi ya vizazi vya sasa na vijavyo kwa maendeleo ya taifa.

No comments:

Post a Comment