Chanzo ni BBC Swahili
Mmarekani mwenye asili ya Afrika, Amina Wadud - ambaye alichagua kuandika jina lake kwa herufi ndogo, kulingana na herufi za Kiarabu ambazo hazitambui herufi kubwa - alikuwa mwanamke wa kwanza kuongoza sala ya Ijumaa nchini Marekani na Uingereza mwaka 2005 na 2008.
Jina lake linajulikana na wengi kama Bibi Imamu.
Hata hivyo, muda mrefu kabla ya hapo, mwaka 1992 alikuwa amepata mafanikio kwa kuandika kitabu cha Quran na Mwanamke.
Katika kitabu hicho, Amina anafasiri Quran kwa mtazamo wa wanawake kuhusu mada mbalimbali, kama vile umuhimu wa wanawake katika Quran, na pia nafasi na haki za wanawake katika Uislamu.
''Sifanyi hivyo ili kuwa wa kwanza katika jambo lolote, au kuwa kiongozi kwa yeyote. Bali ninajali sana uhusiano wangu na Quran na jinsi unavyotofautiana na ukweli ninaoupata, kwa mfano katika jamii ya Kiislamu," alisema Amina.
![]() |
Amina Wadud aliandika kitabu cha Quran na Mwanamke miaka 30 iliyopita, mpaka sasa kitabu chake bado ni kinachapishwa kwa lugha nyingine |
Sasa anachagua kukaa Indonesia.
Kwa BBC Indonesia na mwandishi wa BBC aliyebobea katika masuala ya kidini huko Beirut, Lebanon, Amina alishirikisha safari yake kuelekea Uislamu na juhudi zake za kufikia haki ya kijinsia.
Sio tu kwa wanawake na wanaume bali pia wasiokuwa wawili katika muktadha wa Uislamu.
"Nitasherehekea miaka 70 ya kuzaliwa mwaka huu, pamoja na miaka 50 tangu kuukubali Uisilamu," alisema.
''Ninajihisi mwenye bahati sana, nilipata kitu ambacho nilikipenda, na miaka 50 baadaye upendo na haiba haijawahi kufifia.''
Alizaliwa katika familia ya wachungaji nchini Marekani
Niliingia kwenye makazi ya Amina huko Yogyakarta, nikakaribishwa na meza iliyokuwa mbele ya lango la kuingilia iliyokuwa ikionyesha vitu mbalimbali.
''Mimi ni Muislamu ambaye mawazo yangu yanachangiwa na vyano mbalimbali,'' alisema Amina, ambaye alichagua kuandika jina lake kwa herufi ndogo zote, kwa sababu alisema Kiarabu haitambui herufi kubwa.
Juu ya meza kuna fuwele, kadi za ubashiri, ishara ya mti wa uzima katika Ubuddha, ishara ya kidini ya Kiyahudi yenye jina la mjukuu wake ambaye ni wa asili ya Kiyahudi, na picha za mama na dada yake ambao wamefariki dunia.
"Napenda kupamba meza hii kulingana na nguvu ninayotaka kujisikia siku hiyo," alisema Amina.
"Ninaweka meza baada tu ya mlango ili kuwe na mtiririko wa nguvu fulani kulingana na feng shui."
Uwazi wa Amina kwa utofauti wa mila, dini na desturi umeonekana tangu alipokuwa anakua.
Alizaliwa katika familia ya wachungaji Wakristo wa Methodisti katika jimbo la Maryland, Marekani.
Hata hivyo, kabla ya kuingia kwenye Uisilamu, Amina alikubali na kufuata Dini ya Buddha.
''Baba yangu alinilea kwa upendo," Amina aliniambia na mwandishi wa BBC mjini Beirut, Lebanon, ambaye alijiunga na mahojiano kupitia mtandaoni.
''Kwa hiyo sijawahi kuwa na uzoefu mbaya ambao ulinifanya kuhisi haja ya kutafuta njia nyingine [za kidini]. Lakini nina shauku kubwa katika tofauti za kidini," aliendelea Amina.
Dini ya Haki katikati ya Udhalimu
Alipokuwa na umri wa miaka 19, katika mwaka wake wa pili wa chuo, 1972, Amina alisema hukumu mbili za imani hiyo katika msikiti usio mbali na nyumba ya wazazi wake huko Washington, DC.
Harakati za haki za kiraia za asili ya Kiafrika huko Marekani ziliweka historia katika maisha ya Amina wakati huo.
''Katika jumuiya ya Wamarekani wenye asili ya Afrika, kulikuwa na uelewa wa Uislamu kama mbadala wa mtindo wa Kikristo, ambao ulikuwepo wakati huo, ambao ulikuwa muhimu katika utumwa wa Waafrika,'' Amina alisema.
Kwa mujibu wa Amina, jamii ya Wamarekani wenye asili ya Afrika inauona Uislamu kuwa ni dini ya uadilifu katikati ya dhuluma kwa kuzingatia rangi ya ngozi zao wakati huo.
Hata hivyo, Amina pia hakatai kwamba ubaguzi wa rangi haukukoma tu baada ya kuingia kwenye Uisilamu.
''Sisi, kwa njia nyingi, hatujui ukweli kwamba ingawa hakuna uhalali katika Uislamu kwa ubaguzi wa rangi, bado kuna ubaguzi ndani ya jamii ya Kiislamu,'' aliendelea Amina.
Data ya Kituo cha Utafiti cha PEW mwaka wa 2019 inaonyesha kuwa watu wa asili ya Kiafrika ni moja ya tano ya jumla ya Waislamu nchini Marekani.
Karibu nusu ni waongofu.
''Nilipoanza kuingia kwenye Uislamu, nilifikiria kwa nini tu nisijaribu.''
''Sikutambua ilikuwa ahadi ya maisha,'' Amina anasema huku akicheka.
Kuwa Imamu wa sala ya Ijumaa
2008
Amina Wadud ana shahada ya udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Michigan, Marekani kwa masomo ya Kiarabu na Kiislamu.
Pia alisoma Kiarabu katika Chuo Kikuu cha Marekani huko Cairo, Misri, pamoja na Mafunzo ya Quran na Tafsir katika Chuo Kikuu cha Al-Azhar, Misri.
Alianza utafiti wa kitabu chake, Quran na wanawake, kama sehemu ya tasnifu yake tangu miaka ya 1980.
''Nilijifunza Kiarabu kama ufunguo wa mlango wa kuelewa [Quran], sio kama mlango,'' Amina alisema.
Tangu kuchapishwa kwake miaka 30 iliyopita, kitabu cha Quran na Mwanamke kimetafsiriwa katika angalau lugha saba, ikiwa ni pamoja na Kiindonesia.
Ndani yake, Amina anaandika: Kinachonitia wasiwasi zaidi kuhusu tafsiri za kijadi ni kwamba zimeandikwa na wanaume pekee.
Ina maana kwamba uzoefu wa wanaum unahusika [katika tafsiri], na uzoefu wa wanawake unaweza kutengwa, au kufasiriwa kupitia maono, mitazamo, na mapenzi ya wanaume.
''Mawazo mengi yamejikita kwenye sayansi ya tafseer. Sisemi kila kitu ni kibaya, na mimi pekee ndiye ninayeifasiri Quran vizuri, hapana,'' alisema Amina.
''Namaanisha, siwezi kuona, katika fasihi hiyo, uhalisia wa maisha yangu kama mwanamke Mwafrika mwenye asili ya Kiafrika akielezewa kwa uzito sawa na mwanaume,'' Amina alisema.
Jina la Amina lilijulikana zaidi mwaka wa 2005 baada ya kuongoza maombi ya Ijumaa kwa makutaniko ya wanaume na wanawake huko New York, Marekani.
Wakati huo, alijikuta katikati ya wanaomsema vizuri na wale wanaomsema vibaya.
Lakini hilo halikumzuia kufanya vivyo hivyo mwaka 2008 katika msikiti mmoja huko Oxford, Uingereza.
''Nina upendo, napenda kupendwa, na bila shaka nampenda Mungu wangu kipenzi. Kwa hiyo, hapana, sikusudii kuwa na utata,'' alisema Amina.
''Hata hivyo, ninaelewa kwamba baadhi ya vipengele [kama vile] ustawi wa binadamu, kujiheshimu, haki, heshima, usawa, havina masharti. Ukiweka masharti kwa wanawake au wasio na wawili kupata ukamilifu kama binadamu, mimi huwa nashikilia msimamo wangu dhidi yake.''
Ingawa msukumo wa Amina katika kuandika kitabu cha Quran na Mwanamke ulikuwa umejaa maadili ya usawa wa kijinsia, alikiri kwamba wakati huo hakujiona kama mwanamke, na hata alielekea kukataa lebo hiyo.
Kadhalika anapoongoza Sala ya Ijumaa.
Ninahisi kuwa sihitaji kitu kingine zaidi ya Uislamu na ninaendelea kujiendeleza, kujifunza na kuukubali Uislamu,'' alisema Amina.
Alikubali tu neno la kuwa kwenye harakati za kutetea wanawake mwaka 2009, katika uzinduzi wa vuguvugu la kimataifa la Waislamu la usawa na haki liitwalo Musawah.
Imani ya Kiislamu haiyumbishwi miaka 50 baadaye
Hadi sasa, Amina bado anafanya mazoezi ya kutafakari.
Pia anatumia meza niliyoiona nyumbani kwake kama madhabahu ya kuonyesha vitu vinavyoashiria maisha yake na nguvu anayotaka kuleta.
Amina aliiambia BBC kuwa alijiruhusu kukumbatia urithi wake wa kiroho.
Pia anajiona kuwa ni Mwislamu tofauti, maana yake ni mchanganyiko wa mambo.
"Nimefika mahali ambapo uhusiano wangu na Mwenyezi Mungu upo karibu kiasi kwamba hakuna mambo ya kidunia yanayoweza kuniondoa kwenye ibada na upendo huo," alisema Amina.
''Hata nikihisi mila nyingine takatifu ni sehemu ya maisha yangu, haitishi imani yangu ya Kiislamu. Bado naamini kwamba hakuna mungu isipokuwa Allah, Muhammad ni mjumbe wa Allah...''
CHANZO NI BBC SWAHILI
No comments:
Post a Comment