BASHE-NFRA ANZENI MARA MOJA KUNUNUA MAHINDI KUTOKA KWA WAKULIMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, May 24, 2022

BASHE-NFRA ANZENI MARA MOJA KUNUNUA MAHINDI KUTOKA KWA WAKULIMA



Na Okuly Julius-Dodoma 

WAZIRI wa kilimo Hussein Bashe amewaagiza Wakala wa Taifa wa hifadhi ya chakula (NFRA) kuanza kununua mahindi kwa wakulima pamoja na kufungua vituo sehemu mbalimbali hapa nchini kwa ajili ya kununua mahindi katika mikoa ambayo msimu wa mavuno umeanza.

Mhe.Bashe ameyasema hayo 23,Mei 2022 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maagizo hayo aliyoyatoa huku akisema kuwa msimu huu NFRA wanatakiwa kuwahi kununua Mahindi tofauti na ilivyozoeleka kuwa mpaka ifikapo mwezi wa 7 na 8 ndio wanaanza kununua mahindi.

" Nimewaagiza NFRA kuanza mara moja kununua mahindi kuanzia tarehe 24,Mei 2022 na nawaelekeza kufungua vituo kwa ajili ya kununua Mahindi kutoka kwa wakulima" Amesema

Akaongeza "Na muhakikishe mnapeleka bei shindani katika soko namaanisha bei iliyopo sokoni ili mkashindane na wafanyabiashara ambao nao wapo wananunua mahindi na niwakumbushe tu kuwa katika mikoa kama Rukwa na Katavi tutakutana na msukumo mkubwa hasa kwa wafanyabiashara kutoka nchi za jirani kwa sababu asilimia kubwa ya jirani zetu hawana chakula cha kutosha" amesema Bashe

Bashe amesema kuwa serikali mwaka huu imepanga kununua tani laki moja za mahindi huku akiwatoa shaka wanachi kuwa mpaka sasa kuna chakula cha kutosha hivyo hakuna dalili yeyote ya njaa nchini.

Pia amewaagiza NFRA kuhakikisha wanafungua maduka katika wilaya ya Bunda kwa ajili ya kuwauzia wananchi mahindi kutokana na uhaba wa chakula wilayani humo na kusababisha mahindi kuuzwa bei kubwa kulinganisha na maeneo mangine hapa nchini.

Pia amewaomba wananchi kuhakikisha wanahifadhi mazao kwa ajili ya chakula huku akisisitiza kuwa hata kama watafanyabiashara ya mahindi wafanye lakini wabakize chakula kwa ajili ya familia zao.

"Siwakatazi kuuza mahindi yenu na hatuna mpango wowote wa kufunga mipaka ila niwaombe wananchi uzeni Mazao yenu ila muhakikishe mnabakiza chakula cha kutosha kwa ajili ya familia ni aibu kubwa sana kulima na kuuza mahindi yote alafu baadae unaanza kununua tena chakula"Amesema Bashe

No comments:

Post a Comment